Wasanii
na wadau wa tasnia ya filamu wanaoshiriki kikao kazi cha kuandaa rasimu ya sera
ya filamu wakifurahia jambo na mwandishi mkongwe wa riwaya na miswada ya filamu
Amri Bawji (mwenye baraghashia). Kikao kazi hicho kinafanyika ukumbi wa
mikutano wa Taasisi ya Sanaa Bagamoyo (TaSUBA)
KILIO cha muda mrefu cha wadau wa sekta ya filamu
nchini sasa kinaelekea kupata ufumbuzi wa kudumu baada ya Bodi ya Filamu
Tanzania kuwakutanisha wadau wake kwa ajili ya maandalizi ya sera mahususi
itakayotoa mwongozo na kuendeleza sekta hiyo nchini.
Sekta ya filamu nchini imekuwa ikisimamiwa na Sera ya Utamaduni na Sheria ya Filamu na
Michezo ya kuigiza Na. 4 ya mwaka 1976
pamoja na kanuni zake. Kukosekana kwa sera mahususi ya filamu nchini kuliibua changamoto
mbalimbali. Changamoto hizo ni pamoja na kuwepo kwa filamu na michezo mingi ya
kuigiza inayotayarishwa chini ya viwango, kutokuwepo kwa mitaji na uwekezaji wa
kutosha, sekta ya filamu kutoendeshwa kibiashara, kukosekana kwa mifumo bora ya
usambazaji, kutokuwepo kwa weledi na ubunifu wa kutosha, uharamia wa kazi za
filamu n.k.
Changamoto zilizoainishwa hapo juu zilibainika baada
ya Bodi ya Filamu Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kufanya tafiti
kuhusu hali halisi ya tasnia (situational analysis) na kuuwasilisha mbele ya
kikao kazi cha wadau kilichofanyika tarehe 3 Oktoba, 2016 ukumbi wa uwanja wa
Taifa. Kwenye kikao hicho, Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Nape Nnauye, aliagiza uongozi wa
Bodi ya Filamu Tanzania na wizara yake kushirikiana pamoja kuhakikisha sera
mahususi ya filamu inapataikana mapema iwezekanavyo.
Sera hiyo mahsusi ya filamu nchini inategemewa kuwa
mwarobaini wa changamoto zinzoikabili sekta hiyo kwa muda mrefu sasa. Ikumbukwe
wadau wa tasnia ya filamu nchini wamekuwa wakilalamika kukosa mapato stahili yanayotokana
na kazi zao, kushindwa kupata mitaji ya kuwawezesha kuwekeza miundo mbinu ya
kisasa kwenye uzalishaji na mfumo hafifu wa kupambana na uharamia wa kazi zao.(Picha zote na Habari na Ofisi ya Mawasiliano na Uhusiano Bodi ya Filamu Tanzania)
|
No comments:
Post a Comment