TANGAZO


Wednesday, November 9, 2016

KONGAMANO LA NISHATI TANZANIA, DK. PALLANGYO AELEZA MIKAKATI YA SERIKALI KUZALISHA UMEME

Baadhi ya washiriki wa Kongamano wakifuatilia Majadiliano. 
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo akifungua rasmi Kongamano la Ufunguaji wa Milango ya Uwekezaji katika Sekta ya Nishati Tanzania jijini Dar es Salaam leo. 
Washiriki wa Kongamano wakiendelea na majadiliano. Wa kwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Decklan Mhaiki akifuatiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga akifuatiwa na Mwakilishi kutoka Nedbank Afrika Kusini, Michael Creighton. 
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (katikati) akiagana na Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa TIB Development Bank, Joseph Chilambo (kushoto). Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Umeme, Mhandisi Innocent Luoga. 
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa tatu kulia) katika picha ya pamoja na waandaaji wa Kongamano. Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya ATI na Kamishna wa Bima Tanzania, Israel Kamuzora akifuatiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Dkt. Gideon Kaunda, Mkurugenzi Mkuu Wakala wa Bima ya Biashara Barani Afrika (ATI), George Otieno na wa kwanza kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Umeme, Mhandisi Innocent Luoga. 
Washiriki wa Kongamano kutoka Wizara ya Nishati na Madini wakifuatilia majadiliano. Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, katikati ni Mhandisi Neema Rushema akifuatiwa na Mhandisi Ahmed Chinemba.

Na Mohamed Seif, Nishati na Madini
KATIKA kukidhi mahitaji ya umeme na nchi kuwa ya viwanda kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, Serikali imeamua kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo wakati akifungua Kongamano lililofanyika jijini Dar es Salaam likihusu Ufunguaji wa Milango ya Uwekezaji katika Sekta ya Nishati ili kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo nchini.

Alitaja baadhi ya miradi hiyo ni ya kufua umeme ikiwemo upanuzi wa mradi wa Kinyerezi I (MW 185) na Mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi II (MW 240).

“Miradi mingine tunayotekeleza ni ya usambazaji umeme ikiwemo laini ya Iringa –Shinyanga yenye msongo wa kV 400, Arusha – Singida yenye msongo wa kV400, na Dar es Salaam- Chalinze – Tanga –Arusha wa msongo wa kV 400,” aliongeza Mhandisi Pallangyo.

Alisema kuwa kwa sasa kiasi cha umeme kilichopo kwenye gridi ni megawati 1,357.69  ambapo umeme unaotokana na chanzo cha maji unachangia asilimia 41.7%, gesi asilia 44.7%, mafuta mazito 12.8% na tungamotaka 0.8%. 

Aliongeza kuwa umeme unaopatikana nje ya gridi ni megawati 82.28 na kwamba mpaka sasa asilimia 40 ya wananchi nchini ndiyo wanaopata huduma ya umeme.

Alisema kuwa miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya wananchi wanaotumia umeme na kuongeza kuwa mahitaji ya umeme nchini yanakadiriwa kukua kwa asiliamia 10 hadi 15 kwa mwaka.

Aidha alisema kuwa ili kutimiza lengo la kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025, Serikali imelenga kuongeza uzalishaji wa umeme hadi kufikia megawati 5000 ifikapo 2020 na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.

“Sasa ili kutimiza lengo hilo la kuwa na megawati 10,000 ifikapo 2025 inahitajika kuwa na mtaji mkubwa ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali kama ya usambazaji na usafirishaji umeme hivyo ni muhimu kwa Serikali kushirikiana na kampuni binafsi katika kutekeleza hayo,” alisema Mhandisi Pallangyo.


Kongamano hilo liliandaliwa na Wakala wa Bima ya Biashara Barani Afrika (ATI) na kuhudhuriwa na wawekezaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, Taasisi za Kimataifa, Wizara na  Taasisi mbalimbali za Serikali ambapo masuala mbalimbali kuhusu na Nishati yalijadiliwa.

No comments:

Post a Comment