Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo
Na Beatrice Lyimo-Maelezo, Dodoma
09/09/2016
SERIKALI imeanza kutatua changamoto za umeme katika mikoa ya
Lindi na Mtwara kwa kuiunganisha mikoa hiyo kwenye umeme wa gridi ya taifa kupitia
njia ya KV 400.
Akijibu swali la Mhe. Vedasto Ngombale lililohusu kiini cha
ukatikaji wa umeme leo mjini Dodoma, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter
Muhongo amesema kuwa suala la umeme kutoka Lindi hadi Mtwara linachangamoto
nyingi za kiufundi ambapo hupelekea tatizo hilo kijitokeza.
Prof. Muhongo amesema kuwa mitambo ya Somangafungu
inachangamoto kwani umeme unaofuliwa kutoka mitambo hiyo unatumika katika
Wilaya za Kibiti, Kilwa na Rufiji ambapo hutumia Megawati 7.5 kwa kutumia gesi
asilia.
Aidha, Serikali kupitia Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO)
imeanza ukarabati katika Wilaya za Kibiti, Kilwa na Rufiji wa mitambo miwili
yenye uwezo wa kuzalisha umeme kwa jumla ya Megawati 5 unaotarajiwa kukamilika
Novemba, 2016 na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 3, ambapo ufufuaji wa
mtambo wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2.5 unategemewa kuanza mwezi Oktoba
mwaka huu.
Kwa upande mwingine Naibu Waziri wa Nishati na Madini Medard
Kalemani amesema kuwa Serikali imeanza utekelezaji wa ujenzi wa njia ya umeme
itakayounganisha Wilaya ya Liwale na Nachingwea ambapo kwa sasa zinatumia umeme
kutoka kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia kilichopo Mtwara.
Naibu Waziri huyo, amesema kuwa hatua iliyofikiwa kwa mpango
huo ni ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa KV 33 yenye urefu wa Kilomita 14.5
kutoka Nachingwea hadi kijiji cha Luponda na kilomita 73 kutoka Liwale hadi
kijiji cha Nangano kuelekea Nachingwea.
Zaidi ya hayo, TANESCO inaendelea na ukaguzi, usafirishaji na
ukarabati wa miundombinu ya kusambaza umeme kwa lengo la kuwaondolea wananchi
kero ya kukatika kwa umeme hatua ambayo itaondoa tatizo katika maeneo hayo.

No comments:
Post a Comment