KUONDOA Watumishi wasiostahili katika orodha ya malipo ya
mshahara Serikalini ni kazi endelevu na inafanyika kwa kushirikiana na waajiri
nchini. Katika makala hii Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) anaongea kuhusu hatua
mbalimbali na kazi zilizofanywa na Ofisi yake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki
(Mb) alisema hayo hivi karibuni katika kipindi cha mahojiano ya moja kwa moja
katika Runinga ya Taifa (TBC) na kusisitiza waajiri wanawajibu wa kuondoa
mtumishi yeyote asiyestahili mara moja.
“Tumefanya zoezi mahsusi
kuwaondoa kwenye orodha ya malipo ya mishahara watumishi wasiostahili.
Watumishi wanaoondolewa ni wale walioacha kazi, kufukuzwa kazi, kumalizika kwa
muda wa ajira ya mkataba na kugombea nafasi za kisiasa. Kuanzia tarehe 01
Machi, 2016 hadi tarehe 20 Agosti, 2016 jumla ya watumishi 16,127 wameondolewa
na wasingeondolewa kwa wakati wangeisababishia Serikali
hasara ya Shilingi 16,014,697,390 kwa mwezi mmoja” Mhe. Kairuki aliainisha.
Alisema hatua
zinachukuliwa kwa wote waliobainika kuhusika katika suala hilo ambapo hadi
tarehe 20 Agosti, 2016 jumla ya watumishi 839 walifikishwa Polisi na
TAKUKURU ili kutoa maelezo; na uchunguzi unaendelea hatimaye hatua za
kisheria zichukuliwe kulingana wa ushahidi utakaopatikana.
Waziri Kairuki alisema
lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba fedha zote zilizolipwa kwa watumishi
wasiostahili zinarejeshwa Serikalini akibainisha kuwa toka mwezi Machi, 2016
hadi mwezi Julai, 2016 jumla fedha zilizorejeshwa ni Shilingi 14,403,046,089.27
na zoezi ni endelevu.
Waziri Kairuki alisema
Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCIMS) unaimarishwa kulingana na
mahitaji na kutaja maeneo yaliyoimarishwa ikiwamo; Uwezo wa kutambua na kuzuia
kuajiriwa watu wenye majina yanayofanana; Kuongeza moduli ambayo inamwezesha
mwajiri kufanya uhakiki wa watumishi kwa kutumia taarifa mbalimbali zikiwemo za
Kitambulisho cha Taifa;
Uwezo wa kuwaondoa kwenye orodha ya malipo ya mishahara
watumishi waliofikisha umri wa kustaafu na ambao hawana mikataba; Kuongeza
Moduli ya Utambuzi wa Kituo cha Kazi cha mtumishi (Service Delivery Point)
na hilo limeanza kwa Idara za Afya, Elimu, Kilimo na Mifugo; na Wigo wa
matumizi ya mfumo umepanuliwa ili kuwawezesha Wakuu wa Idara za Afya, Elimu
(Sekondari/Msingi), Kilimo na Mifugo kutumia na kuona taarifa za watumishi
walio chini yao.
Akiongea kuhusu mkakati wa kuboresha Maadili katika Utumishi wa
Umma alisema pamoja na mambo mengine Serikali inasimamia kukuza
uelewa wa Maadili kwa Watumishi wa Umma kupitia mafunzo na kuendeleza ushiriki
wa Asasi za Kiraia (AZAKI) katika kuhamasisha wananchi kuzingatia maadili na
kuacha kutoa vishawishi kwa watoa huduma. Pia, kuhakikisha kila Taasisi ya Umma
ina Mkataba wa Huduma kwa Mteja na dawati la kupokea, kushughulikia malalamiko
na kutoa mrejesho kwa wananchi.
Waziri Kariuki aliongeza
pamoja na ofisi yake kuhakikisha Watumishi wa Umma wanatoa Kiapo cha
Ahadi ya Uadilifu na kusimamia viapo hivyo, pia inaandaa Mfumo wa Kielektroniki
unaojulikana kama “Watumishi Portal” ambao utakuwa na moduli
ya kupokea malalamiko, maoni na kero mbalimbali kutoka kwa Watumishi wa Umma na
kuhamasisha Taasisi za Umma kuwa na kituo mahususi cha utoaji huduma (One
Stop Service Centre) ili kupunguza kero kwa wananchi wanaofuata huduma.
Eneo la Uwajibikaje hali
ikoje?
Waziri Kariuki alisema Serikali imekuwa na utaratibu wa kupima
utendaji wa Mtumishi Mmoja mmoja kwa kutumia Mfumo wa Wazi wa Mapitio na
Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS).
Hata hivyo, alisema “Serikali inalenga kuimarisha mfumo wa
uwajibikaji katika ngazi ya Taasisi ili kuhakikisha Taasisi za Umma
zinatekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kuanzisha Mfumo wa Mikataba ya Utendaji
Kazi katika Taasisi zote za Umma kuanzia mwaka wa fedha 2017/18”.
Alifafanua kuwa Mkataba
huo ni makubaliano ya kimaandishi kati ya Taasisi za Umma na Serikali ambayo
yatatekelezwa na Taasisi husika katika kipindi cha mwaka mmoja na Mkataba utajikita katika kupanga
na kupima utendaji wa Taasisi na utakuwa na malengo,
shabaha, vigezo na viashiria vya utendaji ambavyo vitatekelezwa na Taasisi
katika mwaka husika.
Waziri Kairuki alianisha
kuwa Mkataba huo utaainisha wajibu wa Serikali katika kuwezesha Taasisi kufikia
malengo na shabaha na utekelezaji wake utafanyiwa tathmini kila mwisho wa mwaka
na matokeo yake kutangazwa kwa umma.
Miongoni mwa faida za
mfumo huo ni kuziwezesha Taasisi za Umma kuimarisha uchaguzi wa vipaumbele
katika ngazi ya Taasisi na upangaji mipango ya utekelezaji kila mwaka;
kuimarisha ufuatiliaji na upimaji utendaji kazi; na kuimarisha uwajibikaji na
uwazi.
Usimamizi wa Maadili kwa viongozi wa Umma
ukoje?
Itaendelea IJUMAA IJAYO
No comments:
Post a Comment