“MALI
ZILIZOPATIKANA KWA NJIA YA RUSHWA NA UFISADI KUTAIFISHWA...
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akiongea na vyombo vya habari kuhusu masuala ya Utumishi wa Umma nchini Tanzania hivi karibuni. (Picha ya Maktaba).
MAKALA iliyopita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki
(Mb) aliongea kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
Serikalini, pamoja, Matumizi ya Nyaraka za Serikali na Maadili kwa viongozi kwa
viongozi wa Umma. Waziri Kairuki aliongea hayo katika Runinga ya Taifa (TBC),
makala ya leo ni sehemu ya mwisho na inaangalia mapambano dhidi ya rushwa na
mpango wa kunusuru kaya masikini hapa nchini.
Mapambano
dhidi ya rushwa
Waziri
Kairuki alieleza Serikali imekuwa ikichukua hatua katika kuzuia na kupambana na
rushwa nchini mfano kwa kufuatilia
fedha za Miradi ya Maendeleo kupitia Ofisi za Kanda za TAKUKURU kwa lengo la
kuhakikisha thamani ya miradi inayotekelezwa inaendana na kiasi cha fedha kilichotolewa
ambapo ufuatiliaji huo umeiwezesha Serikali kuokoa kiasi cha Shilingi Bilioni
39.34.
“Tumewasilisha
majalada 297 kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa ajili ya kuombewa kibali
cha mashitaka ambapo majalada 229 yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani”
Waziri Kairuki alifafanua.
Aliongeza
mikakati ya serikali ni pamoja na kuhuisha Sheria ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa
Na. 11 ya 2007 ili kujumuisha makosa ya uhujumu uchumi na kutaifisha mali zilizopatika
na kwa njia ya Rushwa na Ufisadi.
Kuhusu kaya masikini hali ikoje?
Waziri
Kairuki alisema Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ambao
utachukua miaka kumi unatekelezwa katika Halmashauri zote za Tanzania Bara
pamoja na Zanzibar.
“Katika kipindi cha miaka minne
mpango umetekelezwa Vijiji, Mitaa na Shehia 9,960 ambayo ni sawa na wastani wa
asilimia 70. Kaya 1,358,268 zimetambuliwa ambapo kati ya hizo, Kaya 1,110,377
zimeandikishwa” Waziri Kairuki alisena na kuongeza kaya 1,110,377
zimehawilishiwa fedha kwa kulipwa ruzuku katika awamu 16 ili kuziwezesha
kuwekeza katika lishe, afya na elimu.
Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi
unatekelezeka?
Waziri Kairuki alisema Mpango
wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership) ulianza kutekelezwa nchini toka mwaka
2012/13, na umejikita katika kuweka uwazi zaidi katika uendeshaji wa shughuli
za Serikali; Ushirikishwaji wa Sekta za Umma na Binafsi katika utekelezaji wa
Mpango; Uwajibikaji wa Serikali kwa Wananchi; Matumizi ya Teknolojia na
Ubunifu; na Mapambano dhidi ya Rushwa.
Alisema miongoni mwa yaliyofanyika ni
pamoja na kuongezeka kwa uwazi kuhusu bajeti ya Serikali kwa kuandaa kijitabu
cha “Citizen
budget” kilichoandaliwa kwa Kiswahili na
lugha rahisi kwa kuchapishwa kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha na
Mipango. Pia, taarifa za utekelezaji za sekta za kipaumbele Afya, Elimu na Maji
kuchapishwa katika Tovuti za sekta hizo na kukamilika kwa zoezi la upembuzi
yakinifu wa Takwimu Huria (Open Data)
ili kuongeza uwazi wa takwimu na taarifa
mbalimbali;
Waziri
Kairuki alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Uendeshaji wa
Shughuli za Serikali kwa Uwazi kwa mikakati mbalimbali ikiwamo, kuendelea na
utekelezaji wa kuwa na uwazi katika bajeti ya Serikali kwa kuweka taarifa za
bajeti kwenye tovuti mbalimbali kwa lugha nyepesi na kwa Kiswahili na
kuimarisha mfumo wa Takwimu Huria ambayo utarahisha wadau mbalimbali kupata
takwimu zinazohusu masuala mbalimbali hususan Afya, na Elimu.
Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
(OR-MUUUB) ina majukumu ya kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Sera za
Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma; Taratibu, Miundo na Mifumo
ya Utoaji Huduma; Uendelezaji Rasilimaliwatu; Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka
katika Utumishi wa Umma. Aidha, Ofisi hii inasimamia maadili ya Watumishi na
viongozi wa Umma; mapambano dhidi ya
rushwa; Mfuko wa Maendeleo ya Jamii; Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na
Biashara za Wanyonge; Mfuko wa Rais wa Kujitegemea; na Taasisi ya Uongozi.


No comments:
Post a Comment