TANGAZO


Saturday, August 13, 2016

WAENDELEZA SEKTA YA MILIKI WAOMBWA KUWEKEZA DODOMA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi

Na Jonas Kamaleki, MAELEZO
WAENDELEZAJI Sekta za Miliki nchini wameombwa kuwekeza Dodoma ili kuweka mazingira safi ya Serikali kuhamia mjini hapo.

Akizungumza na Waendelezaji sekta za miliki (Real Estate Developers) leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amewakaribisha waendelezaji hao kuanza uwekezaji wa majengo mjini Dodoma.

“Sisi tuhahamia Dodoma tunawaomba nanyi watu wa sekta binafsi kuwekeza mjini hapo ili kushirikiana na Serikali katika zoezi hilo. Dodoma kuna fursa nyingi za biashara hivyo nawataka kazichangamkie”,alisema Lukuvi.

Aidha, Lukuvi amesema kuwa Dar es Salaam itakuwa ni kitovu cha biashara na si kwa ajili ya  shughuli za kiserikali, hivyo itakuwa na sura tofauti ambayo itaakisi kuwa ni kweli ya kibiashara.

“Tunatengeza mpango kamambe (Master plan) wa jiji la Dar es Salaam ili kiwe kweli kitovu cha biashara, hiyo ni fursa nyingine kwenu kuitumia”,alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, mpango huo wa Dar es Salaam mpya utakamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu (2016) na utaenda sanjari na wa jiji la Mwanza na Arusha.

Akiwakaribisha waendelezaji wa sekta za miliki, Lukuvi amesema Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) imeshapima na kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli mbali mbali mjini Dodoma. Ameainisha maeneo hayo kuwa ya makazi, shule, viwanda, Hospitali, Mahoteli na sehemu za starehe.

Rai ya Waziri Lukuvi inakuja siku chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipotoa kauli kuwa Serikali itahamia Dodoma ndani ya kipindi chake cha uongozi kilichobaki cha miaka mine (4) na miezi mine (4).

Tamko la Rais Magufuli alilolitoa wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Julai 23, 2016, lilifuatiwa na la Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ambaye alisema kuwa yeye atahamia Dodoma Septemba, 2016. Baada ya hapo mawaziri kadha wa kadha wameonyesha kuunga mkono tamko hilo na kuanza kujiwekea malengo ya kuhamia Dodoma.

Tangu nia ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Serikali itolewe mwaka 1973 na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, maandalizi ya kuhamia huko ndipo yalianza. 

Majengo kwa ajili ya ofisi za serikali yalianza kujengwa na kuthibitisha hilo baadhi ya wizara zilionyesha nia ya kuhamia Dodoma. Mpaka sasa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa iko Dodoma na nyingine zinafuata.

No comments:

Post a Comment