Mbunge wa Bunda Ester Bulaya
Na Immaculate Makilika-Maelezo
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jimbo la Bunda Bi. Janeti Mayanja amepokea madawati 90 yalitolewa na Mbunge wa Jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bi. Ester Bulaya, ambapo hapo awali madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo hilo walikataa kupokea madawati hayo baada ya kuwa yameandikwa jina la mbunge huyo pamoja na kuwa yamenunuliwa na fedha za Mfuko wa Jimbo.
Akizungumza leo kwa njia ya simu, Mkurugenzi Mayanja alisema kuwa amepokea madawati hayo jana Agosti 12 kutoka kwa Mbunge wa jimbo hilo Ester Bulaya baada ya kufutwa jina lake, ambapo madawati hayo tayari yamewasilishwa katika shule tatu zilikuwa na uhaba.
“Tulifanya kikao na Mbunge Bulaya na tukakubaliana kuwa ni vyema majina yake yakafutwa katika madawati hayo kwa vile yalinunuliwa kwa fedha za Mfuko wa Jimbo, lakini endapo mbunge atapenda kutupa madawati atakayonunua kwa fedha zake binafsi na kuandika majina yake hapo tutapokea kwa vile bado kuna tunauhitaji katika jimbo letu” alisema Mkurugenzi Mayanja.
Alifafanua kuwa fedha zilizotumika kununulia madawati hayo zilikuwa ni fedha za Mfuko wa Jimbo zinazotokana na ruzuku ya Serikali ambazo matumizi yake hupangwa na Ofisi ya Mbunge.
Madawati hayo 90 yalisambazwa katika shule tatu za Msingi zilizopo katika Jimbo la Bunda zilizokuwa na uhaba wa madawati ambazo ni Nyatwali, Nyerere na Ligamba, zilizopewa madawati 30 kwa kila moja.
No comments:
Post a Comment