TANGAZO


Tuesday, August 16, 2016

CBE, TFDA NA AFRICAN RELIEF ORGANISATION WAMKABIDHI MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM PAUL MAKONDA SH. MILIONI 31.7 ZA MADAWATI LEO

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dk. Emmanuel Munishi (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda (kushoto) Mfano wa hundi ya shilingi milioni 8,000,000/= zilizotolewa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kama mchango wa chuo hicho kwa jamii kwa ajili ya kununulia madawati yatakayotumiwa na wanafunzi wa shule za msingi katika mkoa huo.Katikati ni Afisa Uhusiano wa Jamii wa Chuo hicho Leonidas Tibanga.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dk. Emmanuel Munishi (katikati) akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kukabidhi mchango wa wa madawati wa shilingi milioni 8 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda (kulia) leo jijini Dar es salaam. Mchango huo umetolewa na chuo hicho kununulia madawati yatakayotumiwa na wanafunzi wa shule za msingi za mkoa huo, Kushoto ni Afisa Uhusiano wa Jamii wa Chuo hicho Leonidas Tibanga.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Hiiti Sillo (kulia) akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 17,700,000/= Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (kushoto) kama mchango wa madawati kwa wanafunzi wa shule za Msingi jijini Dar es salaam leo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda (kushoto) akiangalia mfano wa hundi ya shilingi milioni 6 zilizotolewa na Taasisi ya Kijamii inayojihusisha na masuala ya Kijamii ya African Relief Organisation ya jijini Dar es salaam kwa ajili ya kununulia madawati. Kulia ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Shekh Abdallah Ndauga na Mratibu wa Miradi wa Taasisi hiyo Moadh Shannawi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kupokea msaada wa Fedha kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Taasisi ya Kidini ya Masuala ya Kijamii ya African Relief Organisation kwa ajili ya kununulia madawati kwa shule za Msingi za Dar es salaam. (Picha/Aron Na Aron Msigwa – Dar es salaam)

MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ametoa wito kwa Taasisi na Mashirika mbalimbali jijini Dar es salaam kujitokeza kwa wingi kuunga mkono zoezi la uchangiaji wa hiari wa madawati kwa shule za msingi linaoendelea jijini humo ili kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia yatakayozalisha  wanafunzi bora wa shule za msingi.
Akizungumza mara baada ya kupokea mchango wa fedha za kununulia madawati kiasi cha shilingi milioni 31.7 kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Taasisi ya kidini ya masuala ya jaamii ya African Relief Organisation leo jijini Dar es salaam Mhe. Makonda amesema kuwa bado jamii inao wajibu  na jukumu la kuhakikisha kuwa mazingira ya kusomea ya wanafunzi wa shule za msingi yanakuwa bora ili kuzalisha wahitimu walio na msingi imara.

“Napenda kutumia fursa hii kuzishukuru taasisi hizi ambazo zimeitikia wito wa kutoa michango yao ili kuwezesha upatikananji wa madawati, nawashukuru sana viongozi wa taasisi hizi kwa kuitikia wito wa mkoa wetu na kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuhakikisha shule zetu zina madawati na hakuna mwanafunzi anayekaa chini” Amesisitiza Makonda.

Ametoa wito kwa wananchi ambao wanaguswa kwa namna moja au nyingine  kuendelea kutoa michango yao ili kuwasaidia wanafunzi wa shule za Msingi katika jiji la Dar es salaam ambao walikuwa wanapata shida ya kusomea katika mazingira magumu.

Ameongeza kuwa ili taifa liweze kuwa na wataalam wazuri katika Nyanja zote lazima msingi wa elimu katika shule za msingi uwe mzuri na kufafanua kuwa ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na mkoa wa Dar es salaam ni kukamilisha upatikanaji wa madawati na majengo ya madarasa.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dkt. Emmanuel Munishi akizungumza mara baada ya kukabidhi mfsno wa hundi ya shilingi milioni 8 kama mchano wa chuo hicho kwa jamii amesema kuwa wao kama Chuo cha Elimu ya Biashara chenye kampasi mikoa minne ya Tanzania ukiwemo Mwanza, Dar es salaam, Dodoma na Mbeya kimeguswa kuchangia kiasi hicho cha fedha kwa kuwa kinawategemea wanafunzi waliofundishwa vizuri kutoka shule za Msingi.

Amesema wameamua kuunga mkono Juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ili kuhakikisha kuwa shule Zote za Dar es salaam zinaondokana na shida ya madawati.

“Sisi tumeguswa na uchangiaji wa madawati kwa kuwa ni taasisi ya ya elimu ya juu, kama taasisi ya elimu ya juu hatuwezi kupata wanafunzi wetu kama hakuna shule za msingi, tumeamua tusiwe watu wa kuvuna tu tukaamua kwenda moja kwa moja kwenye msingi ili kujenga msingi imara wa shule zetu” Amesisitiza.

Ameziomba taasisi zote za Elimu ya juu nchini kuiga mfano wa CBE katika kuchangia sekta ya elimu hapa nchini.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Kidini ya Masuala ya Kijamii ya African Relief Organization ya jijini Dar es salaam Shekh Abdallah Ndauga iliyochangia shilingi milioni 6 amemshukuru Mkuu wa Mkoa huo kwa moyo wake wa kuendelea kuwahamasisha wananchi ambao wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kuchangia madawati.

Amsesema Taasisi ya African Relief Organisation itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na mkoa wa Dar es salaam katika kuleta maendeleo ya wananchi wake kupitia miradi mbalimbali wanayotekeleza ikiwemo uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali nchini.

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Hiiti Sillo akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada uliotolewa na Mamlaka hiyo wa shilingi milioni 17.7 amesema TFDA inaunga mkono jitihada za Rais, Dkt. John Pombe Magufuli za kuhakikisha kuwa kila mtoto anakaa katika dawati ambapo katika bajeti yake ya mwaka 2015/16 inatoa mchango wa madawati 236.

Sillo ameongeza kuwa TFDA pamoja na majukumu iliyonayo inatambua kuwa elimu ndiyo nguzo muhimu katika kupambana na maadui wakubwa wa maendeleo, hivyo itaendelea kutoa mchango wake katika kusaidia sekta ya elimu hapa nchini.

No comments:

Post a Comment