Miongoni mwa habari nyingine kuu leo, Bi Hillary Clinton ameidhinishwa kuwa mgombea urais wa chama cha Democratic na Rais wa Brazil aliyesimamishwa kazi Dilma Rousseff ahatahudhuria sherehe za ufunguzi wa michezo ya Olimpiki.
1. Clinton aidhinishwa kuwa mgombea wa Democratic
Bi Hillary Clinton mkewe Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, amekuwa mwanamke wa kwanza kupeperusha bendera ya chama kikubwa nchini Marekani baada ya kuidhinishwa na chama cha Democratic kuwania nafasi ya urais.
Wajumbe katika mkutano wa kitaifa wa Chama uliofanyika katika mji wa Philadelphia, wamemteua rasmi mwanamke huyo aliyekuwa Seneta na waziri wa mambo ya nje kama mgombea wao wa urais. Dakika chache zilizopita mumewe Bi Clinton alimaliza kulihutubia mkutano huo wa wajumbe.
Katika siku ya mwisho hapo kesho, Rais Barrack Obama na Bi Hillary Clinton watakuwa wazungumzaji wakuu katika mkutano huo wa wajumbe mjini Philadelphia.
2. Hollande asema tishio la ugaidi limezidi Ulaya
Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema kuwa tishio la magaidi wa Kiislamu inayokabili bara Ulaya kwa sasa, halijawahi kushuhudiwa kwa kiwango cha sasa.
Akiongea baada ya wanachama wa itikadi kali ya jihadi kumuua kinyama kasisi mmoja ndani ya kanisa lake, Bw Hollande ameelezea azma yake ya kushinda ugaidi, lakini akaongeza kuwa, polisi tayari wana nguvu ya kutosha kukabiliana nao.
3. Macri kukabili unyanyasaji wa wanawake Argentina
Rais wa Argentina, Mauricio Macri, ametangaza mipango mipya ya kukabiliana na dhuluma dhidi ya wanawake.
Bw Macri amesema kwamba elimu ni nguzo muhimu ya kumaliza kabisa unyanyasaji utokanao na tamaduni potovu, iliyokithiri katika jamii ya makabila ya taifa hilo, dhidi ya wanawake.
4. Wabunge Uingereza wataka uamuzi kuhusu raia wa EU
Kamati moja ya Bunge nchini Uingereza, imependekeza kuwekwe tarehe ya mwisho kwa raia wa muungano wa mataifa ya Umoja wa Ulaya (EU) wanaoingia nchini Uingereza chini ya sheria ya sasa. Ripoti ya kamati hiyo inasema kuwa raia wa EU wanaoishi Uingereza kabla ya tarehe iliyowekwa, wana haki ya kuwa wakazi ya kudumu.
5. Rousseff asema hatahudhuria Olimpiki
Rais wa Brazil aliyesimamishwa kazi, Dilma Rousseff amesema kuwa hatahudhuria sherehe za ufunguzi wa mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika mjini Rio, kwa sababu hayuko tayari kudunishwa uwanjani Maracana.
Msemaji wa Rais wa mpito, Michel Temer, amesema kuwa Rouseseff anatarajiwa, kuketi katika viti vilivyoko chini yake na wala sio karibu naye katika jukwaa moja.
6. Roger Federer kukosa Olimpiki
Na Roger Federer amejiondoa kushiriki mashindano ya Olimpiki na mashindano mengine ya tenisi msimu huu, kwa sababu ya jeraha la goti.
Anasema kuwa anahitaji muda zaidi kupona kufuatia upasuaji aliyofanyiwa mapema mwaka huu.

No comments:
Post a Comment