Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga
Na Lilian Lundo – Maelezo
10/06/2016
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewataka watanzania kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yanayoadhimishwa Juni 16, kila mwaka.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Sihaba Nkinga imeeleza kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuwa na siku maalum ya kuelimisha na kuwakumbusha wazazi, walezi na wadau mbalimbali kuitikia utekelezaji wa wajibu na majukumu yao katika kuwapatia watoto haki zao za msingi.
“Tarehe 16 Juni ya kila mwaka, ni kilele cha maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika, katika siku hii, Tanzania inaungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Afrika kuadhimisha siku hii kwa mujibu wa Azimio lililopitishwa na nchi 51 za Umoja huo mwaka 1990,” imefafanua taarifa hiyo.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa Azimio hilo lilipitishwa kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya watoto wa shule yaliyofanyika katika kitongoji cha Soweto, Afrika ya Kusini Juni 16, 1976, ambapo watoto wapatao 2,000 waliuawa kikatili na Makaburu wakiwa katika harakati za kutetea haki zao za msingi za kutobaguliwa kutokana na rangi yao.
Katika siku hiyo watoto hupata nafasi maalum ya kujieleza, kusikilizwa, kushirikina kuonyesha vipaji vyao mbele ya wazazi, walezi na jamii kwa ujumla. Watoto wanahaki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na kutobaguliwa
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni “Ubakaji na Ulawiti kwa Watoto Vinaepukika: Chukua Hatua Kumlinda Mtoto.”
No comments:
Post a Comment