Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo
Na Ismail Ngayonga, Maelezo, Dodoma
8.6.2016
SERIKALI katika mwaka wa fedha 2016/17 imepanga kukarabati miundombinu ya halmashauri mpya 20 za Wilaya nchini ili kusaidia kuboresha mazingira ya kufanyia kazi katika ofisi hizo.
Katika ukarabati huo, Serikali imepanga kutumia Tsh. Bilioni 2 katika kila Halmashauri ya Wilaya hizo.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mhe. Amina Makalagi, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo alisema adhma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa Ofisi na nyumba za Watumishi zinajengwa katika Wilaya na Mikoa mipya nchini.
Mbunge huyo wa Viti Maalum alitaka kujua mikakati ya Serikali ya kuimarisha miundombinu ya Halmshauri mpya zilizoanzishwa hivi karibuni.
Naibu Waziri Jaffo alizitaja halmashauri mpya za Wilaya zitakazoboreshewa miundombinu ya Ofisi zake kuwa ni Kibiti, Malinyi, Buchosa, Madaba, Mpimbwe, Msimbo, Kakonko, Kyerwa, Uvinza, Chemba, Busega, Itilima, Ikungi,na Songwe.
Aidha Jaffo alizitaja halmashauri nyingine kuwa ni pamoja na Chalinze, Ifakara, Newala, Mbulu, Mbinga, Nzega, na Kasulu.
Kwa mujibu wa Jaffo pamoja na ukarabati wa miundombinu ya halmashauri hizo mpya, Serikali pia imekusudia kutumia kiasi Tsh Milioni 500 hadi Milioni 850 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya halmashauri za Wilaya zilizokuwepo hapo awali ili ziendelee ktuoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Josephine Chagula, Jaffo alisema katika mwaka wa fedha 2014/15 Serikali ilipeleka kiasi cha Tsh. Milioni 450 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi katika makao makuu ya Wilaya hiyo.
Aliongeza kuwa kati ya fedha hizo Tsh. Milioni 177 zimetumika kwa ajili ya kumlipa mtaalam mshauri ambaye ni BJ Amli LTD kwa ajili ya kuandaa michoro, upembuzi yakinifu na usanifu wa eneo lote zitakazojengwa Ofisi.
Mbunge huyo alitaka kufahamu mpango wa haraka wa Serikali wa kuwezesha ofisi na nyumba za watumishi katika makao makuu ya Wilaya eneo la Karumwa.
SERIKALI NA WADAU WA MAENDELEO WATENGA DOLA BILIONI 3.3 KUTEKELEZA AWAMU YA PILI YA PROGRAMU YA SEKTA YA MAJI NCHINI
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe
Na Ismail Ngayonga, Maelezo, Dodoma
8.6.2016
SERIKALI kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imepanga kutumia kiasi cha Dola Bilioni 3.3 ili kutekeleza awamu ya pili ya programu ya maendeleo ya sekta ya maji nchini 2016/17 hadi 2020/21.
Akijibu Swali la nyongeza la Mbunge wa Buhingwe (CCM), Albert Obama, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe, alisema awamu ya pili ya programu hiyo tayari imeanza mwezi Januari mwaka 2016.
Kamwelwe alisema Wizara yake itahakikisha kuwa inaajiri wataalamu wa kutosha ili kila Halmashauri iweze kutelekeleza programu hiyo kwa mafanikipo makubwa zaidi.
“Pale ambapo halmashauri yeyote itakuwa na tatizo la ukosefu wa watumishi, Wizara yangu itatuma wataalamu wake katika halmashauri hiyo ili kuhakikisha kuwa wananchi wetu wananufaika na programu hiyo” alisema Kamwelwe.
Mbunge huyo wa Buhingwe alitaka kufahamu ni lini programu ya mradi wa maji katika jimbo la Buhingwe utaanza kutekelezwa.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge huyo, Kamwelwe alisema kutokana na ahadi aliyoitoa Rais Dkt. John Pombe Magufuli Serikali ilituma pesa katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe kiasi cha Tsh. Milioni 10 kwa ajili ya kufanya usanifu wa mradi.
Aidha aliongeza kuwa kutokana na andiko la ukarabati wa mradi huo kugharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 1, Serikali ilipanga kuutekeleza mradi huo katika awamu ya pili ya programu ya maendeleo ya sekta ya maji.



No comments:
Post a Comment