SERIKALI YAWATAKA WENYEVITI WA SERIKALI ZA VIJIJI KUTANGAZA TAARIFA ZA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA SERIKALI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene.
Na Ismail Ngayonga, Maelezo, Dodoma
SERIKALI imewataka Mwenyekiti wa Serikali za Vijiji nchini kutangaza na kuweza wazi taarifa za mapato na matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo katika kipindi cha kila baada ya miezi mitatu (3).
Hatua ya kutotangaza taarifa hizo itaondoa uhalali wa mikutano mikuu unaohitajika kuitishwa na Viongozi hao katika kipindi hicho, kama inavyoelekezwa katika sheria ya fedha ya mamlaka ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982.
Hayo yamesemwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene wakati wa mahojiano yake na waandishi wa habari waliotaka kufahamu umuhimu wa wananchi wa vijijini kuifahamu bajeti ya Serikali.
Simbachawene aliwataka Viongozi waliopo katika mamlaka ya Serikali za Mitaa wakiwemo Madiwani kusimamia kikamilifu suala hilo ili kuhakikisha kuwa wananchi waliowachagua wanafahamu matumizi ya fedha mbalimbali zinazotumwa na Serikali katika Halmashauri za Wilaya.
“Wapo baadhi ya Wenyeviti wamekuwa wakificha taarifa hizo kutokana na maamuzi yasiyo ya busara katika matumizi ya rasilimali ikiwemo uuzaji wa ardhi, hatua inayopelekea migogoro ambayo kimsingi haina umuhimu wowote” alisema Simbachawene.
Kwa mujibu wa Simbachawene alisema Mwenyeviti wa Mitaa, Vijijini na Vitongoji hawana budi kutambua kuwa dhana ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi pamoja na mambo mengine inawahimizia viongozi hao kutoa taarifa hizo katika kipindi kilichowekwa kwa mujibu wa sheria.
SERIKALI YATENGA BILIONI 2.7 KUTANGAZA UTALII NDANI NA NJE YA NCHI
Na Ismail Ngayonga, Maelezo Dodoma
SERIKALI kupitia Bodi ya Utalii Nchini (TTB) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), katika mwaka 2016/17 imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 2.7 kwa ajili ya kuitangaza sekta ya utalii ndani na nje ya nchi.
Akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum (CCM), Maria Kangoye, leo Bungeni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani alisema bajeti hiyo ni ongezeko la asilimia 14.7 za fedha za Serikali zilizotengwa katika bajeti ya mwaka ya 2015/16.
Makani alisema Serikali itaendelea kuboresha sekta ya utalii kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo na vyanzo vingine vya mapato kama ilivyoanishwa katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano 2016/17- 2020/21.
Alisema Serikali pia imepanga kuimarisha Chuo cha Utalii katika kampasi za Bustani iliyopo Dar es Salaam, Temeke na Arusha ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi na umahiri wa wakufunzi, kuboresha upatikanaji wa vifaa vya kufindishia na kuboresha miundombinu ya kampasi hizo.
“Kuhusu uimarishaji wa miundombinu, Wizara yangu imetenga jumla ya Tsh. Milioni 500 katika bajeti ya mwaka 2016/17 ili kukamilisha ujenzi wa jengo la Utalii katika Bustani ya Chuo cha Utalii Tanzania” alisema Mhandisi Makani
Aidha Mhandisi Makani alisema kuwa Chuo cha Utalii Tanzania kwa kushrikiana na Chuo cha Vancouver University cha Canada kupitia mradi wa ISTEP uliopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Ufundi kitaanzisha mafunzo ya Uongozi katika shahada kuanzia mwezi septemba 2018.
Aidha Mhandisi Makani alisema Serikali inaendelea kuelekeza nguvu katika vyuo vilivyopo kwa kuongeza idadi ya wahitimu wa ngazi ya kati na baadaye wa ngazi ya shahada, ambapo kwa sasa Chuo cha Utalii Tanzania kitaanza kuboresha utoaji wa mafunzo katika tansia za ukarimu na Utalii katika ngazi ya shahada.
SERIKALI YASEMA KISIWA CHA SHUNGIMBILI KILICHOPO WILAYA YA MAFIA, PWANI HAKIJAUZWA
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani
Na Ismail Ngayonga, Maelezo Dodoma
SERIKALI imesema kisiwa cha shungimbili kilichopo Wilayani Mafia mkoani Pwani hakijauzwa kwa kampuni ya Zululand ya Afrika Kusini na badala yake kimeingizwa katika uwekezaji kupitia kampuni ya Thanda Tanzania Ltd inayojenga hoteli ya kitalii.
Akijibu swali la Mbunge wa Mwanakwerekwe (CCM), Ali Said Khamis, leo Bungeni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani alisema Alisema uwekezaji huo umepitia taratibu zote za Serikali na pindi utakapokamilika mwekezaji atatekeleza wajibu wake ikiwemo kulipia tozo zote kwa mamlaka zinazohusika kwa mujibu wa sheria.
Makani alisema alisema kisiwa cha shungimbili ni miongoni mwa visiwa 15 ambayo ni maeneo tengefu yanayosimamiwa na Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu nchini (MPRU).
Mhandisi Makani alisema MPRU iliianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge na.29 ya mwaka 1994 ambapo miongoni mwa majukumu yake ni kusimamia maeneo yote yaliyotangazwa kuwa hifadhi za Bahari na maeneo tengefu ya bahari.
Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa ndiyo yenye dhamana ya kuingia mikataba yote ya kimataifa yenye maslahi kwa Taifa.
Aidha akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Singida, Martha Mlatta, Makani alisema Serikali inaendelea kuvijengea uwezo vyuo vya utalii vilivyopo nchini ili kuhakikisha kuwa wahitimu wake wanakuwa mahiri katika soko la ajira nchini.
“Mfanyabiashara akitafuta mwajiriwa ni lazima ahakikishe kuwa anaye mwajiri anakuwa na sifa zote za kumletea faida, hivyo na sisi pia tunataka wahitimu wetu katika vyuo vya utalii wanakuwa wanapata umahiri wa kutosha ili waweze kuajiriwa katika nafasi za juu kabisa katika kampuni yoyote” alisema Makani.
Mbunge Mlatta alitaka swali lake la nyongeza alitaka kufahamu Serikali ina mikakati ipi katika kuhakikisha kuwa wahitimu wa Tanzania wanapewa nafasi za juu za kazi katika hoteli za kimataifa.



No comments:
Post a Comment