Mkurugenzi Msaidizi Usanifu wa Miji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Immaculata Senje.
Na Jacquiline Mrisho-Maelezo
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeazimia kupima jumla ya viwanja 2180 katika Kijiji cha Chasimba, wilayani Kinondoni baada ya kuisha kwa mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na Kiwanda cha Saruji (Twiga Cement).
Hayo, yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Usanifu wa Miji wa Wizara hiyo, Bi.Immaculata Senje alipokuwa akifafanua juu ya malalamiko ya wananchi kuhusu kukosa huduma za umeme na maji katika eneo hilo.
“Baada ya kupatikana kwa suluhisho la mgogoro huu, zoezi la upimaji viwanja linaendelea ambapo hadi sasa tumeshapima jumla ya viwanja 370 kati ya viwanja 2180 vinavyotarajiwa kupimwa kwenye Kijiji hicho,”alisema Bi Senje.
Bi Senje aliongeza kuwa kazi ya kupima viwanja hivyo ilianza mwezi Agosti mwaka jana baada ya Wizara kuunda timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA), Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili waweze kutambua mipaka ya eneo kwa ajili ya kuweka miundombinu.
Aidha, Bi. Senje amesisitiza kuwa wananchi wawe wavumilivu kwani huduma za miundombinu kama vile maji, umeme na barabara zitawekwa baada ya upimaji wa viwanja hivyo kukamilika.
Mgogoro huo ulimalizika mnamo Juni 13 mwaka jana baada ya uongozi wa Wizara kuweka kikao na uongozi wa Kiwanda cha Saruji pamoja na wananchi wa Chasimba ambapo uongozi wa Kiwanda ulikubali kuachia sehemu ya ardhi ambayo ilishaendelezwa na wakazi wa eneo hilo kwa makubaliano ya kupewa fidia na Wizara.
No comments:
Post a Comment