Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia hoja za Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani), wakati wa mkutano wa baraza hilo tarehe 9 Aprili, 2016 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Dkt. Hamis Mwinyimvua akizungumza wakati wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Waziri Mkuu, Aprili 9, 2016 Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (wanne kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi hiyo mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo Aprili 9, 2016.
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
WATUMISHI wa Ofisi ya Waziri Mkuu wametakiwa kuwa wabunifu katika sehemu zao za kazi ili kuongeza ufanisi katika majukumu yao ya kila siku.
Akitoa wito huo wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu,Bunge, Ajira,Kazi na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema watumishi wanatakiwa kutumia rasilimali walizonazo kuonesha ubunifu wao katika idara na vitengo walivyopo ili kuongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi wa kila siku.
“Ofisi ya Waziri Mkuu ni mratibu na msimamizi wa shughuli za kila siku za Serikali hivyo basi naomba tuwe wabunifu katika sehemu zetu za kazi ili tumsaidie Mhe. Waziri Mkuu kutelekeza majukumu haya kwa kasi na ufanisi unaotakiwa.” Alisema Mhe. Jenista.
Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa wakuu wa Idara na Vitengo kushirikiana na watumishi katika ofisi zao ili kuongeza ufanisi wa kazi za kila siku katika idara na Vitengo mbalimbali.
Akizungumza mara baada ya kikao Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu Dkt Hamis Mwinyimvua amesema kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi ni fursa muhimu kwa wafanyakazi kukutana na kujadili masuala mbalimbali ili kupata mbinu za kupambana na changamoto zinazokabili Idara na vitengo mbalimbali.
Kwa mujibu wa Waraka wa Rais Namba 1 wa Mwaka 1970, moja ya madhumuni ya kuanzishwa kwa Mabaraza ya Wafanyakazi ni kuongeza ufanisi na tija katika sehemu za kazi na kupitia Mabaraza haya, wafanyakazi pamoja na waajiri hupata fursa ya kubadilishana mawazo na kubuni mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto katika sehemu zao za kazi.
No comments:
Post a Comment