Pages

Friday, April 1, 2016

STAMICO YAJIZATITI KUUBORESHA MGODI WA TANZANITE

Baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Nishati na Madini wakiwa tayari kuwaongoza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kushuka chini ya ardhi kunakochimbwa madini ya Tanzanite walipokuwa katika ziara kukagua Mgodi wa Tanzanite One hivi karibuni. Kutoka Kulia ni Fundi Sanifu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) Zakaria Mtunya, Afisa wa Bunge kutoka Wizarani Amon Marco, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini Elias Kayandabila na Mhandisi Nyanswi Mbona (TMAA). 
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Zena Kongoi (wa pili kutoka kulia) akiwa na baadhi ya Wajumbe wanawake wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, muda mfupi kabla ya kushuka chini ya ardhi kwa kutumia Kiberenge maalumu ili kujionea mahala kunakochimbwa madini ya Tanzanite.
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Zena Kongoi, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Mgodi wa Tanzanite One kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini hivi karibuni. Kamati hiyo ilifanya ziara Mgodini hapo kujionea namna unavyofanya kazi. 
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Ally Keissy, akiuliza swali wakati wa kikao cha majumuisho baada ya ziara ya kamati hiyo katika migodi mbalimbali inayochimba madini ya Tanzanite Mirerani hivi karibuni. 
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Susan Kiwanga, akiuliza swali wakati wa kikao cha majumuisho baada ya ziara ya kamati hiyo katika Migodi mbalimbali inayochimba madini ya Tanzanite Mirerani hivi karibuni.

Na Veronica Simba - Mirerani
IMEELEZWA kuwa, hatua ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico), kuweka wawakilishi wake katika Mgodi wa Tanzanite uliopo katika eneo la Mirerani Kitalu C, imeonesha mafanikio makubwa ikiwemo kupungua kwa wizi wa ndani na kuimarika kwa mifumo ya uendeshaji Mgodi.

Aidha, imeelezwa kuwa katika kipindi cha ubia wa Shirika hilo na Kampuni ya Madini ya Tanzanite One (TML), Juni 2013 hadi Februari 2016, jumla ya karati 30, 674, 250 za Tanzanite zimezalishwa na kuuzwa kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 13.64.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO, Zena Kongoi alisema hayo jijini Arusha hivi karibuni, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika Migodi mbalimbali inayochimba madini ya Tanzanite ukiwemo Mgodi wa Tanzanite One.

Alisema kuwa Mgodi umeweza kuchangia pato la Taifa kwa kurejesha mrabaha wa asilimia Tano (5.0) ya mauzo ambayo ni sawa na Dola za Marekani 481, 271.04 kwa Serikali.

Vilevile, Kongoi alitaja mafanikio mengine yaliyopatikana katika Mgodi huo kwa mwezi Februari mwaka huu kuwa ni  pamoja na kulipa ushuru wa huduma wa asilimia 0.3 ya mauzo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, kiasi cha Dola za Marekani 32, 769.75.

Akielezea zaidi kuhusu utaratibu wa Shirika hilo kusimamia kwa karibu maslahi yake na Serikali kwa ujumla katika kuendesha na kusimamia mradi huo, Mkurugenzi huyo wa STAMICO alisema kuwa kulingana na maeneo ya usimamizi kuwa mengi mgodini, kuanzia mwezi Machi mwaka huu, Shirika limeongeza idadi ya watumishi uangalizi na usimamizi kufikia Sita.

"Awali, tulipeleka Maafisa watatu kufanya kazi hiyo ya uangalizi na usimamizi. Sasa tumeongeza idadi hiyo mara mbili ili kuleta ufanisi zaidi," alisema Kongoi.

Akizungumzia majukumu ya Maofisa hao, Kongoi alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu namba 12 cha mkataba wa kuendeleza Mgodi huo, timu ya wataalam wenye fani mbalimbali iliundwa ikijumuisha wahandisi, wajiolojia, wachenjuaji na wahasibu ambao jukumu lao kubwa ni kufuatilia, kusimamia na kushauri juu ya mwenendo wa uendeshaji wa shughuli za kila siku za Mgodi pamoja na utekelezaji wa masuala ya mkataba wa ubia.

STAMICO iliingia ubia na Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd (TML) mwaka 2013 kwa uwiano wa 50 kwa 50 ili kumiliki leseni ya uchimbaji madini na kuendeleza Mgodi wa Tanzanite katika eneo la Mirerani Kitalu C.


No comments:

Post a Comment