TANGAZO


Monday, March 7, 2016

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi Siku ya Wanawake Duniani

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan

Na Eliphace Marwa -Maelezo
IKIWA ni kuelekea kusherehekea maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani inayosherehekewa Tarehe 8 Machi kila mwaka, Shirika lisilo la Kiserikali la Kazi Services Limited kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri Nchini (ATE) wameandaa semina maalumu itakayofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kazi Services Limited Bi. Zuhura Muro alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu semina hiyo alisema kuwa lengo la maadhimisho haya ni kufurahia mafanikio ya mwanamke katika Nyanja zote za kijamii, uchumi, siasa na utamaduni na ili kufanikisha furaha hiyo wamemualika Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu kuwa mgeni rasmi.
Aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa maadhimisho hayo Taasisi ya Kazi Services Limited kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri Nchini (ATE) kupitia programu ya  Mwanamke wa Wakati Ujao ̋ wameandaa kongamano maalum ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa kwa lengo la kuwajengea uwezo vizazi vijavyo ili Tanzania iwe yenye wanawake wenye uwezo na umakini katika kazi. 

̎̋Tunaposherehekea mafanikio ya mwanamke, tunaboresha taifa letu kwa kujitoana kufanya kazi kwa bidii, hii ni katika ngazi zote makazini iwe kwenye Makampuni, Mahakamani, Jeshini na kwenye kilimo, kote huku tunaboresha nguvu ya mwanamke na kujenga usawa wa jinsia.Tunaleta maboresho haya yote kwa lengo la kumuwezesha mwanamke ̋, alisema Bi. Zuhura.

Jumla ya wanawake zaidi ya 400 kutoka fani na idara mbalimbali kama vile watumishi wa Umma, Jeshi, Sheria, Sekta binafsi na zingine nyingi wanatarajiwa kuhudhuriwa maadhimisho hayo ili kubadilishana mawazo na uzoefu kwa lengo la kuboresha ufanisi wao kwa ujumla.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2016 ni ;̎ Kumuwezesha Mwanamke ili kupata usawa wa kijinsia ̋, kauli mbiu hii inalenga kuamsha na kumuwezesha mwanamke kujitambua na kusimama katika kazi na kujenga Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment