Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
akimwapisha Bw. Alphayo Kidata kuwa Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Na Raymond Mushumbusi- MAELEZO
15/3/2016. Dar es salaam.
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
imekusanya takribani Sh. billioni 12 kutoka kwa wafanyabiashara ambao walikwepa
kodi na kupewa muda wa siku 14 na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kulipa kodi hizo kwenye mamlaka hiyo.
Akitoa takwimu hizo mara baada ya kuapishwa kuwa
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata amesema, kila
Mtanzania ana jukumu la kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na sio kukwepa na
amehaidi kulisimamia vizuri suala la ukusanyaji wa mapato katika sehemu
mbalimbali ili kuongeza mapato ambayo yatasaidia kufanikisha maendeleo katika
sekta mbalimbali.
“Tutajitahidi kwa kila namna kuwaelimisha wananchi
wetu ili wafahamu wajibu wao na umuhimu katika kulipa kodi na sio kukwepa
kulipa kodi na tunawaomba wananchi kila waendapo kupata huduma yoyote ile iwe
katika sekta binafsi au Serikalini basi anatakiwa aombe stakabadhi za
manunuzi au huduma ili tuweze kudhibiti upotevu wa kodi” alisema Kidata.
Kamishna aliongeza kwamba Kidata mamlaka hiyo
ipo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na kama kuna suala lolote au tatizo
kuhusu kodi kuna ofisi katika mikoa yote ikiwa ni hatua ya kutatua shida zao na
kama kuna mtumishi yoyote wa mamlaka hiyo atashindwa kumuhudumia mwanachi inavyotakiwa
basi taarifa zitolewa mara moja kupitia namba zao zilizoko kwenye tovuti ya
mamlaka hiyo, ambayo ni www.tra.go.tz ili kuimarisha huduma zetu kwa wateja.
Aidha Kamishna Mkuu huyo amesema kuwa
watawachukulia hatua wale wote ambao hawatalipa au hawajalipa kodi zao kwa
kuwapeleka mahakamani kwa kukaidi kulipa kodi halali kwa mujibu wa Sheria.


No comments:
Post a Comment