Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania Bwana Sabasaba Moshing akielezea fursa zinazotolewa na taasisi hiyo katika kuwajengea uwezo wananchi kwenye maonesha ya wajasiriamali Michenzani.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania Bwana Sabasaba Moshing akimkabidhi hundi ya shilingi Milioni 15,000,000/- Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif zitakazosaidia harakati za wajasiriamali walioshiriki maonyesho hapo Kisonge Michenzani Mjini Zanzibar.
Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la wajasiriamali Tanzania Zanzibar Bibi Nuru Mohammed akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa maonyesho ya wajasiriamali hapo Michenzani.
Mwenyekiti wa Taifa wa shirikisho la wajasiriamali Tanzania Bwana Masoud Hassan Maftaha akitoa salamu kwenye hafla ya uzinduzi wa maonyesho ya wajasiriamali hapo Michenzani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akikagua kazi mbali mbali zilizotengenezwa na wajasiriamali kutoka mikoa ya Unguja baada ya kuzindua rasmi maonyesho ya wajasiriamali hao.
Balozi Seif akifurahia kazi nzuri iliyofanywa na wana vikundi vya ujasiriamali katika fani ya ushoni kwenye maonyesho ya wajasiriamali hapo bustani ya mnara wa kumbu kumbu ya Mapinduzi Muembe Kisonge Michenzani Mjini Zanzibar.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la wajasiriamali Tanzania { TISF } Nd. Dauda Salmin wa Pili kutoka Kulia akimueleza jambo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya uzinduzi wa maonyesho ya wajasiriamali hapo Michenzani Mjini Zanzibar. Wa kwanza kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Taifa wa shirikisho na wajasiriamali Tanzania Bwana Masoud Hassan Maftaha na wa kwanza kutoka kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa shirikisho na wajasiriamali Tanzania Zanzibar Bibi Nuru Mohammed.
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
5/3/2016.
WAKATI Serikali ikijiandaa kushirikiana na sekta binafsi katika
usajili wa vikundi vyote vya ujasiriamali ili viweze kufanya kazi kwa mujibu wa
sheria na taratibu za nchi, Wananchi na hasa Vijana wanapaswa kuitumia fursa
hiyo kwa kupata ajira ambazo uwezo wa serikali wa kuwaajiri kwa wakati huu ni mdogo.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiyafungua maonyesho ya siku mbili ya wajasiri
amali ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani
yanayofanyika katika bustani ya Mnara wa Kumbu kumbu ya Mapinduzi uliopo Muembe
Kisonge Michenzani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali kupitia Mfuko
wa uwezeshaji iko tayari kuwadhamini wajasiri amali watakaofuzu mafunzo yao
yanatolengwa kutolewa katika Wadi na shehia
zote za Unguja na Pemba.
Alisema Taifa linaelewa changamoto zinazowasumbua
wajasiriamali zikiwemo ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara, mitaji midogo
pamoja na maeneo ya kufanyia biashara zao mambo ambayo yanachangia upatikanaji
mdogo wa ufanisi wa kazi zao.
Balozi Seif alieleza kwamba changamoto hizo
zitafanyiwa kazi na Serikali ili kuiwezesha sekta hiyo binafsi ya ujasiria amali kuwa kimbilio kwa vijana walio
wengi hasa ikizingatiwa uhaba wa nafasi za ajira uliopo Serikalini.
Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inatambua wazi kuwa wajasiriamali ni nguzo imara ya uchumi wa Taifa ikielewa kuwa sekta hiyo ndio mkombozi wa
wananchi walio wengi hapa nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameishukuru Benki ya Posta Tanzania, Benki ya
Wakulima Vijijini (CRDB) pamoja na mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kwa mchango wao wa kusaidia wajasiriamali katika kutatua matatizo yao ya
ukosefu wa mitaji ya kuendesha miradi yao.
Alisema mchango wa Taasisi hizo za kifedha
umedhihirisha wazi jinsi zinavyothamini nguvu
za Wananchi wao wenye juhudi za kujikwamua kimaisha kwa kujishughulisha na kazi
halali za kujiongezea kipato.
Balozi Seif aliwapongeza
waandaaji wa maonyesho hayo ya wajasiriamali yenye kuvutia ambayo yatawasaidia
kuwaelimisha wale waliokuwa wazito wa kujielekeza katika jeshi hilo kubwa la wajasiriamali hapa
Nchini.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania
Bwana Sabasaba Moshing alisema katika
kupiga vita umaskini unaooneka kuiathiri jamii kubwa Nchini Taasisi hiyo ya
kifedha inaendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali kwenye maeneo mbali mbali
nchini kwa lengo la kukabiliana na tatizo hilo.
Bwana Sabasaba alisema Benki ya Posta Tanzania tayari imeshafungua Akauni Elfu
4,000 za vikundi vya vikoba na akauni nyengine 1,000 kwa vikundi visivyo rasmi
kutekeleza azma ya Benki hiyo tokea ilipoanzishwa kwake kwa nia ya kumkomboa
mwananchi.
Akitoa salamu Mwenyekiti wa Taifa wa Shirikisho la
wajasiriamali Tanzania (TISF)
Bwana Masoud Hassan Maftaha alisema Taasisi hiyo inatoa siku 60 kuanzia leo
kuendesha mafunzo bure yatakayowajengea uwezo wa kitaaluma wajasiria amali wa
Zanzibar.
Bwana Masoud alisema Tanzania sio omba omba iwapo mipango
imara itadumishwa katika kuwajengea uwezo wananchi wake hasa
wale walioamua kujikita katika sekta ya ujasiriamali.
Mwenyekiti huyo wa Taifa wa Shirikisho la
wajasiriamali Tanzania alifafanua kwamba wajasiriamali wa Zanzibar lazima
wawezeshwe ili kukidhi mahitaji yao
muhimu pamoja na kwenda sambvamba na mpango huo.
Akimkaribisha mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa
maonyesho hayo ya Wajasiri amali Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana,
Wanawake na Watoto Mh. Zainab Omar Mohammed alisema zipo taasisi nyingi zisizo
za Kiserikali zilizoanzishwa Zanzibar
ambazo tayari zimeshaleta faraja kubwa katika kumkomboa Mwananchi hasa
Mwanamke.
Waziri Zainab aliwataka Wananchi hasa Wanawake na
Vijana kuzichangamkia kwa haraka fursa zote zinazotolewa na taasisi hizo ili
kukabiliana na ukali wa maisha na kupunguza umaskini.
Tanzania hivi sasa ina wanachama wa vikundi vya
ujasiriamali wapatao Milioni 7,284,000 kati ya hao wanachama Laki 100,000 na
vikundi vilivyosajiliwa vipatavyo Elfu 1,213 vipo Visiwani Zanzibar.
Utafiti uliofanya
ndani ya vikundi vya wajasiriamali nchini umebaini kuwa wajasiri wengi
wanafanya biashara zao chini ya kiwango
kinachokubalika cha mtaji, ukosefu wa maeneo ya kufanyia biashara hizo pamoja
na elimu duni ya kuendesha miradi wanayoianzisha.
No comments:
Post a Comment