Utangulizi
Nchi yetu ina kingo za mito na
mabonde na maeneo mengi hatarishi ambamo watu wanaishi kinyume cha sheria, huku
wakiharibu mazingira na kuhatarisha maisha yao.
Kutokana na uhaba wa makazi, hali ni mbaya zaidi katika mabonde ya Jiji
la Dar es Salaam, hasa bonde la Mto Msimbazi.
Serikali za awamu zote, zimekuwa
zikifanya jitihada za kuwaondoa wakazi wa maeneo ya mabondeni wanaoishi katika
maeneo hayo kinyume cha sheria lakini mafanikio yamekuwa si ya kuridhisha.
Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo
moja ya misingi yake mikuu ni utii wa sheria za nchi, imeanza jitihada za
kuwaondoa wakazi hawa. Tuliamua kuanza na Bonde la Mto Msimbazi kwasababu ndiko
kwenye watu wengi na athari kubwa.
Sababu zetu kuu za kufanya zoezi
hili ni kusafisha mabonde na mito katika jiji la Dar es Salaam na mazingira
yanayozunguka ni:-
- Kunusuru maisha ya wananchi
wanaoishi katika mazingira hatarishi. Eneo la Bonde la Mto Msimbazi
lilitangazwa kuwa ni eneo hatarishi kuishi binadamu tangu mwaka 1949 na
baadaye 1979.
- Kupanua uwezo wa mito ya Dar
es Salaam ili kupitisha maji ya mvua kwa kasi kubwa, hivyo kupunguza
uwezekano wa kutokea mafuriko na maafa wakati wa mvua nyingi;
- Kuzuia milipuko ya magonjwa,
hasa ya kipindupindu, hasa wakati wa mvua;
- Kuzuia eneo hilo kuendelea
kutumika kama maficho ya wahalifu na uhalifu;
- Kutoa nafasi kwa Serikali kuandaa na
kuendeleza eneo hilo kwa mujibu wa sheria za nchi na mipango miji;
Utaratibu wa Zoezi
Kabla ya nyumba kubomolewa,
taasisi hizi zinashirikiana kuhakiki iwapo nyumba anayokaa mkazi ina nyaraka za
umiliki na vibali vya ujenzi na iwapo nyaraka hizo zina uhalali wowote. Nyumba
ambazo zimethibitika kuwepo katika maeneo yasiyostahili ndio zinawekwa alama X
kuashiria kwamba wakazi wanapaswa kuhama au kubomoa. Baada ya hapo, mkazi
hupewa muda wa kubomoa na kuhama mwenyewe. Kutokana na utaratibu huu, sehemu
kubwa ya nyumba zinazobomolewa ni zile ambazo watu wamekwishaamua kubomoa
wenyewe. Baada ya hapo, alama huwekwa kuonyesha mpaka wa bonde. Katika zoezi
hili, imebainika kwamba sehemu kubwa ya wakazi wa maeneo ya mabondeni ni
wapangaji huku wamiliki wakikaa sehemu nyingine salama. Serikali pia imeweka
Dawati la Malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Tathmini
ya Zoezi
Jana,
terehe 7 Januari 2016, Mawaziri watatu (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI; na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais; pamoja na Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii), walifanya mkutano wa kutathmini zoezi la kuhamisha
wakazi wa mabondeni katika Jiji la Dar es Salaam.
Mkutano
huo ulipokea ripoti ya timu ya wataalam wa Wizara mbalimbali, inayoongozwa na
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, ambayo, pamoja na mambo
mengine ilibainisha kwamba sehemu kubwa ya kubaini makazi yaliyojengwa kinyume
cha Sheria katika Bonde la Mto Msimbazi imekamilika. Ripoti ilieleza kwamba, hadi
sasa, wananchi katika nyumba 774
wamehama na nyumba hizo kubomolewa. Ilielezwa pia kwamba kabla ya mkazi
kuombwa kuhama, uhakiki kuhusu uhalali
wa makazi anayoishi hufanywa. Kutokana na uhakiki huo, jumla ya wakazi 20
walikuwa na hati halali za makazi na wakazi 119 walikuwa na leseni za makazi za
muda mfupi. Hawa watu hawakuhamishwa. Mawaziri walipokea maelezo kuhusu
changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika zoezi hilo. Baada ya tafakuri na mjadala, Mawaziri hao
walitoka na msimamo ufuatao, kama uamuzi wa Serikali: -
1. Zoezi
la kuwaondoa wananchi waishio katika bonde la Mto Msimbazi (eneo hatarishi)
litaendelea kwa utaratibu ambao hautaleta mateso na usumbufu kwa wananchi;
2. Katika
awamu hii, zoezi litajikita katika Bonde la Mto Msimbazi tu.
3. Kwa
wakati huu, watakaohitajika kuhama ni wale tu ambao makazi yao yamo NDANI
kabisa ya bonde, kwenye miteremko ya kuingia bondeni na kwenye KINGO za mto;
4. Wale
watakaokuwa na nyaraka halali walizopewa na mamlaka za umma, zilizowamilikisha
na kuwaruhusu kujenga katika bonde hilo, hawatahamishwa bila kupewa sehemu
nyingine za kujenga. Na watumishi wa umma waliowamilikisha maeneo hayo
watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria;
5. Serikali,
ndani ya siku tatu zijazo, itaanza zoezi la kuzoa kifusi na kusafisha maeneo
ambapo ubomoaji umefanyika.
6. Serikali
itaheshimu amri za mahakama kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na baadhi ya wakazi
wa mabondeni lakini pia itafuatilia kesi hizi ziishe haraka ili taratibu
zinazofuatia zifanyike;
7. Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu
watumishi wake wanaoendesha zoezi hili kinyume na misingi ya sheria
zinazotekelezwa, na kinyume na misingi ya haki na uwazi, ikiwemo wanaoweka
alama za X zaidi ya mita zilizowekwa kisheria. Limeanzishwa dawati la
malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya
kupokea malalamiko au maswali kuhusu zoezi hili.
8. Nyumba
na majengo ya miaka mingi, yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya kutungwa kwa
Sheria zinazotekelezwa kwa zoezi hili, hayatabomolewa isipokuwa tu pale maisha
ya wakazi yapo hatarini. Wanaoishi katika makazi hayo watapewa miongozo ya
hatua za kuhifadhi mazingira na kujiokoa na maafa;
9. Serikali
haina dhamira ya kubomoa mahoteli makubwa ya siku nyingi yaliyo karibu na fukwe
katika maeneo ya Masaki. Wamiliki wa mahoteli haya watapewa masharti na
miongozo ya kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa Sheria.
10. Serikali
inaweka uratibu wa karibu zaidi miongoni mwa taasisi zake ili hatua za
utekelezaji wa sheria za nchi zisiwe chanzo cha taharuki katika jamii.
11. Serikali
haina dhamira ya kuwatesa wananchi wake kwa kuwalazimisha kuhama katika makazi
yao bila sababu za msingi. Lakini pia Serikali haiwezi kuruhusu wananchi
waendelee kukaa katika maeneo ambayo ikinyesha mvua kubwa maisha yao yapo
hatarini. Itakumbukwa kwamba katika mafuriko ya mwaka 2011, wananchi 49 waishio
mabondeni walipoteza maisha. Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Hali ya
Hewa, mwaka huu zinatarajiwa kunyesha mvua kubwa kuliko zilizowahi kutokea
katika miaka ya hivi karibuni.
12. Serikali
inafuatilia kwa karibu kwa mamlaka za Serikali za Mitaa juu ya taarifa za
wananchi wanaohitaji msaada maalum wa kibinadamu.
Suala la Mchungaji Getrude Rwakatare
Mkutano
ulipokea taarifa kuhusu suala linaloongelewa sana la nyumba ya Mchungaji
Rwakatare. Ilielezwa kwamba Mchungaji
Rwakatare amejenga nyumba yake pahali ambapo amezuia mtiririko wa mto kwa
kujaza kifusi ili kupata eneo zaidi katika eneo la miti ya mikoko, kinyume
kabisa na Sheria tatu muhimu. Pia
ilielezwa kwamba tangu wakati ujenzi unaanza jitihada za kumsimamisha
zilifanyika na mamlaka za Serikali za Mitaa lakini ikashindikana kutokana na
sababu mbalimbali. Pale Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
lilipoingilia kati na kutaka kuibomoa nyumba hiyo, Baraza lilishtakiwa
mahakamani. Wakati kesi inataka kuanza kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa
Baraza, yeye mwenyewe bila kuagizwa wala kuwaarifu wakubwa zake, mnamo tarehe
11 Mei 2015, aliingia makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba
ya Baraza ya kuondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali, kwa niaba ya Baraza,
kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare.
Makubaliano hayo yalisajiliwa na Mahakama kama hukumu tarehe 13 Mei
2015. Mwanasheria huyo alificha makubaliano hayo kwa miezi mitano hadi Oktoba
2015, yalipogundulika na mtumishi mwingine wa Baraza. Mkutano ulielezwa kwamba
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kufuata taratibu zote, alishaagiza
kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mwanasheria huyo.
Mwanasheria huyo alifukuzwa kazi siku ya juzi tarehe 6 Januari 2016 na taarifa
zake zimekwishafikishwa TAKUKURU. Vilevile, Ofisi ya Makamu wa Rais, iliiagiza
Baraza kufungua shauri mahakamani la kuomba “makubaliano” kati yake na
Mchungaji Rwakatare yawekwe pembeni kwasababu yalipatikana na njia ya
udanganyifu. Shauri hilo lilifunguliwa tarehe 29 Disemba 2015.
Kuhusu
Karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Kasi (DART)
Mkutano pia ulijulishwa kuhusu hoja
inayozungumzwa kwamba wananchi wanaondolewa katika maeneo ya kuishi mabondeni
lakini mradi wa DART umeachwa. Mkutano ulielezwa kwamba Sheria ya Mazingira
(kifungu 57 (2)) inatoa nafasi ya kutolewa ruhusa kwa miradi/shughuli zenye
maslahi ya taifa kufanyika katika maeneo ya mabondeni, na kwamba Waziri mwenye
dhamana ya mazingira anaruhusiwa kutoa miongozo ya namna ya shughuli hizo
zinavyoweza kufanyika bila kuathiri mazingira. Mradi wa DART ulipata kibali
hicho na una mkataba na Baraza la Mazingira kuhusu hatua za hifadhi ya
mazingira zinazopaswa kutekelezwa katika mradi huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
08.01.2016

No comments:
Post a Comment