TANGAZO


Sunday, December 27, 2015

Profesa Muhongo awatoa hofu wachimbaji wadogo

Rais wa Wachimbaji wadogo wa Madini Tanzania, John Bina akizungumza wakati wa kikao na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa nne), mkoani Mara jana. 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akizungumza wakati wa kikao chake na wachimbaji wadogo wa madini, Mkoani Mara.

Na Mohamed Seif, Nishati na Madini
SERIKALI imedhamiria kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini nchini ili kukuza uchumi wa Taifa.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema hayo kwenye kikao chake na wachimbaji wadogo wa madini kutoka mikoa ya Simiyu na Mara.

Profesa Muhongo alisema sekta ndogo ya madini nchini inao mchango mkubwa kwenye pato la Taifa wa kuondoa umasikini nchini na hivyo Serikali kwa jitihada mbalimbali itahakikisha wachimbaji wadogo wananufaika ipasavyo pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi.

“Tutawakaribisha wachimbaji wakubwa lakini tunataka na nyie wachimbaji wadogo mchangie ukuaji wa uchumi; mchangie upatikanaji wa ajira kwa vijana wetu,” alisema.

Aliongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa uchimbaji mdogo wa madini, Serikali imeamua na imedhamiria kuwaheshimu na kuwatambua wachimbaji wadogo.

Waziri Muhongo aliwataka wachimbaji hao kubadilika na sio kuendelea kulalamika badala yake wajitume na kufanya kazi kwa uadilifu huku wakitanguliza suala la uzalendo na pia kuamini kwamba Serikali inayo nia thabiti ya kuwasaidia.

Aliwatoa hofu na kuwahakikishia kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuwatafutia maeneo zaidi ya uchimbaji madini na vilevile soko la uhakika ili kuongeza kipato chao na wakati huo huo kuliingizia taifa mapato zaidi.

"Msiwe na wasiwasi, fanyeni uchimbaji wa uhakika; Serikali hii ni yenu; itawasaidia masuala mbalimbali pamoja na kuwatafutia ruzuku, masoko,  mafunzo na pia kuwatafutia maeneo zaidi kwa ajili ya shughuli zenu," alisema.

Aliwataka kuachana na fikra potofu kuwa Serikali haiwajali badala yake waiamini Serikali yao kwamba ipo kwa ajili ya kuwasaidia na huku wakijituma kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uaminifu.

“Matatizo ya zamani ya uchimbaji mdogo tuachane nayo, lazima ulipende taifa lako; huwezi ukawa mchimbaji wa dhahabu ya Tanzania unaipeleka Kenya; halafu inauzwa kama imetoka humo hili ni kosa kubwa,” alisema.

Aliwaasa kuepuka kutorosha madini nje ya nchi; aliongeza kuwa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limepewa jukumu la kuwatafutia bei ya madini kusudi madini yanayopatikana nchini yauzwe nchini na yanunuliwe hapa hapa; iwe ni malighafi ya Tanzania.

Aidha, Profesa Muhongo alimuagiza Meneja wa Tanesco Kanda ya Ziwa Mhandisi Amos Maganga kutembelea maeneo yote ya wachimbaji wadogo ili kujua mahitaji yao ya umeme pamoja na kutathmini namna ya kuwaunganisha na huduma ya umeme.

Aliagiza kuwa baada ya kutembelea maeneo hayo, masuala yanayoweza kutatuliwa hapo kwa hapo lazima yatatuliwe na yale ambayo yatakuwa yanahitaji fedha zaidi wahakikishe wanaweka kwenye mipango ya usambazaji umeme vijijini na iwe kwa ajili ya umeme mwingi wa kuendesha mitambo.

Kwa upande mwingine, wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, wachimbaji hao wadogo wa madini mikoa ya Mara na Simiyu walimpongeza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa juhudi zake katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

Wachimbaji hao walisema uteuzi wa Profesa Muhongo kwenye nafasi hiyo ya Waziri wa Nishati na Madini ni neema kwa sekta hiyo kwani uwepo na umuhimu wake tayari umeonekana.

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji, Rais wa Wachimbaji Wadogo Tanzania, John Bina alisema changamoto zilizokuwa zikiikabili sekta ya madini nchini zimepata tiba.

"Mheshimiwa Rais hakufanya kosa kumteua Profesa Muhongo kwa nafasi hii; anafahamika kimataifa ni mchapakazi. Tulikwisha ona juhudi zake kipindi cha nyuma na sasa amerudi kututumikia," alisema Bina.

Alisema wachimbaji wadogo wa madini nchini wanamuamini Profesa Muhongo na vilevile wanaukubali utendaji wake ambao waliuelezea kuwa ni chachu ya maendeleo kwenye sekta hiyo.

No comments:

Post a Comment