TANGAZO


Friday, November 13, 2015

Wananchi waaswa kupima afya mara kwa mara

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donan Mmbando.

Na Beatrice Lyimo- MAELEZO
13/11/2015
Dar es Salaam.
SERIKALI imetoa wito kwa kila mwananchi nchini kuhakikisha anapima afya yake mara kwa mara kwa kuwa ugonjwa wa kisukari unaweza usionyeshe dalili yoyote mapema ili kukabiliana na kupunguza athari za ugonjwa huo.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Donan Mmbando leo alipokuwa akitoa tamko kuhusu siku ya Kisukari Duniani inayoadhimishwa tarehe 14 Novemba kila mwaka duniani kote. Kauli Mbiu Mwaka huu ni “Ulaji unaofaa, na Kisukari”.

Dkt Mmbando amesema kuwa siku ya Kisukari Duniani ilianzishwa baada ya kuona ugonjwa wa kisukari unaongezeka  kwa kasi Duniani kote,Tanzania kama nchi nyingine huadhimisha siku hii kwa kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania kutoa elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na madhara mbalimbali yatokanayo na ugonjwa huo.

“Ugonjwa wa Kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu” aliongeza Dkt Mmbando.

Mbali na hayo Dkt.Mmbando amebainisha kuwa asilimia 80 ya wagonjwa wa kisukari ulimwenguni wanaishi katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, na tafiti zinaonyesha kuwa mwaka 2007 kulikuwa na wagonjwa 246 Milioni Duniani kote, mwaka 2012 wagonjwa 371 Milioni, mwaka 2013 wagonjwa Milioni 382 ulimwenguni kote ikiwa  wagonjwa Milioni 19.8 kutoka Bara la Afrika.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2012  nchini kwa kuhusisha Wilaya 50 tofauti ulionyesha kuwa asilimia 9.1 ya watanzania wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wana ugonjwa wa kisukari.

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa takwimu za watoto wenye kisukari katika mwaka 2014 ni kati ya asilimia 15 mpaka 20 kwa wagonjwa wote wa kisukari ambao wanatibiwa kwenye Kliniki za hapa nchini.
“Lakini wapo wengine wengi hawajajitokeza kwenye kliniki kwa sababu mbalimbali ikiwemo imani potofu, gharama, pamoja na umbali wa Huduma za Afya zilizopo” aliongeza Katibu Mkuu huyo.

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaendelea na utekelezajiwa Sera ya Afya(2007) inayolenga kutoa huduma kwa magonjwa yasioambukiza ikiwemo Kisukari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Kitaifa na Kimataifa.

No comments:

Post a Comment