Pages

Saturday, November 28, 2015

Wadau wa filamu waiomba Serikali kuanzisha kiwanda cha kuzalisha DVD tupu na vifungashio vya kazi za filamu

Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fisoo (kushoto), akisisitiza jambo wakati wa kongamano la wadau wa filamu lililofanyika Jana Mkoani Morogoro kujadili changamoto na namna ya kukuza tasnia ya filamu nchini.  kulia ni Katibu kutoka Filmmaking Clinic of Tanzania (FCoT) Bw. Ignas Mkindi. 
Katibu kutoka Filmmaking Clinic of Tanzania (FCoT) Bw. Ignas Mkindi (Kulia) akizungumza na wadau wa filamu (hawapo pichani) wakati wa kongamano la wadau hao jana Mkoani Morogoro. Kushoto ni mdau wa filamu na mratibu wa kongamano Bw. Kheri Mkamba. 
Mkurugenzi kutoka Tansquare film house Bi. Christina Mroni akichangia mada wakati wa kongamano la wadau wa filamu lililofanyika Jana Mkoani Morogoro kujadili changamoto na namna ya kukuza tasnia ya filamu nchini. (Picha zote na Genofeva Matemu -Maelezo)

Na Genofeva Matemu - Maelezo, 
28/11/2015.
WADAU wa filamu nchini wameiomba Serikali ya awamu ya tano kutoa kipaumbele kwa viwanda vitakavyofufuliwa kuzalisha DVD tupu na vifungashio vya kazi za filamu vyenye kiwango hivyo kuinua sekta ya filamu kwa kasi.

Rai hiyo imetolewa na mdau wa filamu nchini Bw. Luhende Richard Luhende wakati  wa kongamano la wadau wa filamu lililoudhuriwa na watayarishaji na wazalishaji wa filamu jana Mkoani Morogoro.

Bw. Luhende amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano imelenga kukuza sekta ya filamu kwa kuandaa ilani inayojali wasanii kama ilani hiyo ilivyoainisha katika ukurasa wake wa 219 pamoja na 220.

“Ilani ya chama cha mapinduzi imelenga kukuza sekta ya fulamu hususani katika eneo la miundombinu, ubora na weledi katika sekta na bidhaa zinazozalishwa pamoja na uimarishwaji wa chombo chenye dhamana na filamu kwa maana ya bodi ya filamu, uanzishwaji na uratibu wa mfuko ambao utawawezesha wasanii kupata mitaji hivyo kuzalisha bidhaa zenye ubora” alisema Bw. Luhende.

Aidha Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu bibi. Joyce Fisoo amesema kuwa Serikali imekua ikitoa wito kwa wawekezaji ambao wako tayari kujitokeza kuwekeza katika miundombinu ya filamu hususani jumba changamani la filamu  kwa lengo la kuinua wasanii na kukuza tasnia ya filamu.

Bibi. Fisoo amewataka wasanii kushirikiana, kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na wadau mbalimbali, kujiunga na mafunzo ya muda mfupi kuongeza ujuzi, na kupunguza utamaduni wa kuongelea masuala yasiyokua na tija bali kutumia muda walionao kufanya kazi kwa bidii kama hari iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wa Serikali ya awamu ya tano.


Naye mwakilishi kutoka Proin Promotion Bw. Josephat Lukaza ameipongeza bodi ya filamu kushirikisha wadau wa filamu kwenye matamasha mbalimbali yakiwemo matamasha ya JAMA Festival, Nepal Afrika inayotarajia kufanyika Februari 2016, pamoja na kwenda Misri kwa ajili ya tamasha la Script Writers litakalofanyika Desemba mwaka huu, matamasha ambayo yanatoa fursa kwa wadau wa filamu kupata mbinu mpya za kuendeleza tasnia ya filamu nchini.

No comments:

Post a Comment