TANGAZO


Thursday, November 5, 2015

Urusi na Misri zakerwa na madai kuhusu ndege

Image copyrightAFP
Image captionMaafisa wa Urusi wamekuwa wakichunguza mabaki ya ndege hiyo
Urusi na Misri zimekosoa taarifa zilizotolewa na baadhi ya mataifa kwamba ndege ya Urusi iliyoanguka Sinai na kuua abiria 224 huenda ililipuliwa kwa bomu.
Urusi imesema taarifa hizo ni “uvumi” huku Misri nayo ikisema hakuna “ushahidi” wa kuunga mkono madai hayo.
Maafisa wa Marekani na Uingereza wanasema ripoti za kijasusi zinaonyesha huenda ndege hilo ililipuliwa kwa bomu. Uingereza tayari imesimamisha safari zote za ndege kwenda na kuondoka mji wa Sharm el-Sheikh.
Wanamgambo wa Islamic State wamedai kwamba waliangusha ndege hiyo aina ya Metrojet Airbus 321, iliyokuwa safarini kuelekea St Petersburg.
Ndege hiyo ilianguka katika eneo la jangwa Sinai dakika 23 baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege Sharm el-Sheikh Jumamosi.
Wengi wa waliokuwa kwenye ndege hiyo walikuwa Warusi.
"Hatuwezi tukawa na uhakika kwamba ndege hiyo ya Urusi iliangushwa na bomu lililotegwa na magaidi, lakini dalili zinadokeza huenda hilo ndilo lililofanyika,” alisema Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron.
Bw Cameron na Rais wa Urusi Vladimir Putin wamewasiliana kwa njia ya simu, kwa mujibu wa taarifa ya Kremlin.
Image copyrightReuters
Image captionCameron na Putin wameshauriana kwa njia ya simu
Bw Putin amesisitiza umuhimu wa kutumia data na maelezo kutoka kwa uchunguzi rasmi unaoendelea kubaini chanzo cha kisa hicho.
Marekani ilidukiza mawasiliano na kufikia uamuzi kwamba ndege hiyo ilidondoshwa na kundi la Sinai Province lenye ushirika na kundi la IS, afisa mmoja ameambia AP.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov awali alisema madai yanayotolewa yanaonekana kutolewa kwa kufuata habari zisizothibitishwa au uvumi fulani.
Waziri wa uchukuzi wa ndege wa Misri Hossam Kamal amesema wachunguzi bado hawajapata ushahidi wowote kuthibitisha kwamba ndege hiyo ililipuliwa kwa bomu.
Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi, ambaye kwa sasa yumo kwenye ziara rasmi Uingereza, ambako atakutana na Bw Cameron amesema hawataki “kukimbilia uamuzi.”
"Matokeo ya uchunguzi yatatolewa wazi, hatuna jambo la kuficha.”
Mashirika zaidi ya ndege yameendelea kusitisha safari za ndege Sharm el-Sheikh kama tahadhari, hasa mashirika kutoka Ujerumani, Ubelgiji, Uholanzi, Uingereza na Ireland.

No comments:

Post a Comment