Chama cha upinzani nchini Croatia kinaelekea kupata ushindi mwembamba kwenye uchaguzi wa ubunge uliofanyika Jumapili.
Hata hivyo, hakijapata viti vya kutosha kuunda serikali moja kwa moja.
Matokeo ya awali yanaonyesha chama hicho cha HDZ kitapata viti 60, huku muungano unaotawala wa Social Democrats wa waziri mkuu anayeondoka Zoran Milanovic ukipata viti 50.
Chama hicho cha wahafidhina sasa kinatarajiwa kuanza mazungumzo ya kuunda muungano. Bunge la nchi hiyo huwa na wabunge 151.
Mzozo kuhusu wahamiaji ulikuwa mojawapo ya masuala makuu kwenye kampeni. Zaidi ya wahamiaji 320,000 wamepitia Croatia mwaka huu.
"Ushindi huu umetupa jukumu la kuongoza taifa hilo, ambalo linapitia hali ngumu,” kiongozi wa HDZ Tomislav Karamarko ameambia wanahabari.
“Yeyote atakaye kupigania maisha bora Croatia anakaribishwa.”
Muungano wa gombea huru ambao kwa pamoja umekuwa ukijulikana kama Most (Daraja) ndio uliofaidi zaidi kwenye uchaguzi huo, ukitarajiwa kujizolea viti 19 vya ubunge.
Hata hivyo, muungano huo umesema hautajiunga na mirengo hiyo mingine, mwandishi wa BBC mjini Zagreb Guy De Launey anasema.
Hii ina maana kwamba, iwapo matokeo hayo ya awali ni sahihi, basi huenda hali ya kisiasa isiweze kutabirika.
Mirengo miwili mikuu imekuwa na mitazamo tofauti kuhusu jinsi ya kuwashughulikia wakimbizi na wahamiaji.
Croatia imekuwa ikitumiwa na wahamiaji kutoka Syria, Afghanistan na Iraq wakielekea kaskazini.
Gharama ya kuwashughulikia wahamiaji imefikia £189,000 ($284,000) kwa siku, kwa mujibu wa waziri wa masuala ya ndani wa Croatia Ranko Ostojic.
No comments:
Post a Comment