Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini Bi. Badra Masoud
akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani), mapema leo jijini Dar es Salaam
kuhusu mpango wa Serikali wa kuunda kikosi maalum cha kukabiliana na tatizo la
wizi wa umeme na kuimarisha ukaguzi ili kubaini wateja wasio waaminifu na
kuwachukulia hatua za kisheria. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari
(Maelezo), Bi. Zamaradi Kawawa. (Picha na Fatma Salum- Maelezo)
Na Fatma Salum - Maelezo
SERIKALI inatarajia kuunda kikosi maalum kitakachojumuisha
wataalam kutoka taasisi mbalimbali ili kukabiliana na tatizo la wizi wa umeme
linalopelekea Shirika la Umeme (TANESCO) kukosa mapato inavyostahili.
Hayo yamebainishwa na
Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini Bi. Badra Masoud wakati
akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Bi. Badra amesema kuwa kutokana na wizi wa umeme kukithiri
na kuliingizia hasara Shirika la Umeme (TANESCO),
Wizara itaunda kikosi
hicho kitakachojumuisha wataalam kutoka TANESCO, Wizara ya Nishati na Madini na
Vyombo vya Usalama ili kukabiliana na tatizo hilo.
“Aidha Wizara ya Nishati na Madini imeliagiza shirika la
TANESCO kuimarisha kikosi chake cha ukaguzi wa watumiaji wa umeme ili kubaini
wateja wasio waaminifu wanaoiba umeme na kuwachukulia hatua za kisheria.”
Alisema Badra.
Kwa upande mwingine Serikali imezitaka Taasisi mbalimbali za
Serikali na zisizo za Kiserikali kuzingatia matumizi bora ya umeme ili
kudhibiti upotevu wa nishati hiyo muhimu kwani imebainika kuwa kuna baadhi ya
ofisi wana kawaida ya kuacha wazi vifaa vya umeme baada ya muda wa kazi
vikiwemo vifaa kama kompyuta, AC na taa.
Aidha Bi. Badra ameongeza kuwa Serikali inatoa onyo kwa watu
wanaohujumu miundombinu ya TANESCO ikiwemo kuchoma nguzo za umeme na kuiba
mafuta ya transfoma kuacha mara moja kwani wakigundulika hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi yao.
Akizungumzia hali ya umeme nchini Bi. Badra amesema kuwa
hali ni nzuri na hakuna mgawo wowote kwa sasa kwani kasi ya uzalishaji wa umeme
ni nzuri na kiasi kinachopatikana sasa ni megawati 1500 huku matumizi yakiwa ni
kati ya megawati 800 na 900 kwa siku.

No comments:
Post a Comment