TANGAZO


Wednesday, November 18, 2015

Serikali yaagiza ulinzi shirikishi kwenye Miradi ya Kitaifa

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini (kushoto), Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Paul Masanja (katikati) na Kamishna wa Nishati, Mhandisi Hosea Mbise wakimsikiliza Meneja wa Kampuni ya GASCO, Mhandisi Kapuulya Musomba (hayupo pichani) mara baada ya kufika kwenye Kituo cha Kupokelea Gesi Asilia kutoka Mtwara na Lindi cha Somangafungu. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua Mradi wa Gesi Asilia.

Na Mwandishi wetu
SERIKALI imewataka wasimamizi wa mradi wa Gesi Asilia kushirikiana na vijiji vinavyozunguka na kupitiwa na mradi huo kwenye suala la ulinzi. 

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo na Naibu wake, Mhandisi Paul Masanja walipotembelea Kituo cha Kupokea Gesi Asilia ya Mtwara na Lindi cha Somangafungu (Somangafungu Gas Receiving Station) kilichopo wilaya ya Kilwa, mkoa wa Lindi.

Mhandisi Chambo alisema suala la ulinzi linapaswa kuwa shirikishi na hivyo kuwaagiza kushirikiana na Serikali ya vijiji vilivyo karibu na vituo mbalimbali vya mradi pamoja na vijiji vinavyopitiwa na bomba kubwa la kusafirishia gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

Alisema kwa kushirikiana na wanakijiji suala la hujuma ya miundombinu ya mradi huo halitotokea kwani wanakijiji wanapaswa kuwa sehemu ya mradi.

Alisema mradi huo ni wa wananchi na wanapaswa kushirikishwa aliagiza  kuboreshwa kwa mpango wa uwajibikaji kwa jamii (corporate social responsibility) ili jamii inayozunguka ipate kunufaika na kuulinda mradi huo.

“Wananchi huwa wanahujumu miradi sababu ya kutoona manufaa na miradi husika. Hili sitaki litokee hapa; hakikisheni jamii inanufaika na huduma mbalimbali zinazohitajika na jamii husika,” alisema.

Mhandisi Chambo alisisitiza umuhimu wa utoaji wa taarifa kwa wananchi. Alisema wananchi wanayohaki ya kuelewa kuhusu masuala mbalimbali ya mradi.

“Tumeshuhudia mradi unakwenda vizuri, lakini je wananchi wanapata taarifa hizi?,” alihoji Chambo na kuwataka watumie vyombo vya habari pamoja na vitengo vya habari ili kuwaeleza wananchi kuhusu hatua mbalimbali za mradi.

Kwa upande wake Mhandisi Masanja, alisema suala la ulinzi linapaswa kupewa umuhimu wa kipekee kwani mradi huo umegharimu fedha nyingi lakini pia ni muhimu katika kukuza uchumi na kwa maendeleo ya Taifa.

Alisema mbali na kutumia vyombo vya usalama katika ulinzi wa miundombinu ya mradi huo ni vyema pia wanakijiji wakashirikishwa katika suala zima la ulinzi.

“Wanakijiji ndio wapo huku kwenye mradi na kwenye maeneo linapopita bomba la gesi, kwahiyo ni muhimu sana nao wakawa sehemu ya mradi. Changieni kwenye huduma za kijamii; fanyeni nao vikao kuelewa nini wanahitaji,” alisema Mhandisi Masanja.

Naye Meneja wa Kampuni ya Gesi Asilia (GASCO), Mhandisi Kapuulya Musomba alisema tayari mpango wa CSR upo na unaendelea kufanya kazi na wananchi kwa ukaribu lengo huku lengo likiwa ni kufanya mradi huo kuwa sehemu ya jamii.

“Kwa kupitia mpango tulionao wa CSR tumeweza kusaidia jamii katika masuala mbalimbali. Tumechimba visima kwa baadhi ya vijiji, tumechangia kwenye masuala ya afya. Mpango huu ni endelevu na sio wa mara moja,” alisema.
Katika ziara hiyo, viongozi hao walikagua shughuli mbalimbali ziazoendelea kwenye kituo hicho na kupewa taarifa kuhusu malengo na changamoto za Kituo.

No comments:

Post a Comment