Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama (kushoto), akiwa pamoja na wafanyakazi wa kampuni hiyo, akigawa sehemu ya bidhaa za vyakula, mafuta, sabuni za kufulia, dawa za miswaki na mafuta ya kupakaa, Dar es Salaam leo, ikiwa ni sehemu ya fedha zilizopatikana katika matamasha mbalimbali ya muziki wa Injili yaliyoandaliwa na kampuni hiyo. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Msama Promotions na baadhi ya yatima, wakiwa katika hafla ya ugawaji wa bidhaa za vyakula, mafuta, sabuni za kufulia, dawa za miswaki na mafuta ya kupakaa, yaliyotolewa na kampuni hiyo, Dar es Salaam leo, ikiwa ni sehemu ya fedha zilizopatikana katika matamasha mbalimbali ya muziki wa Injili yaliyoandaliwa na kampuni hiyo.
Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama akiwakabidhi yatima wa Kituo cha Mwandaliwa Orphans, Salma Juma, Mwajuma Hamza na Fahali Haji, sehemu ya bidhaa za vyakula, mafuta, sabuni za kufulia, dawa za miswaki na mafuta ya kupakaa, Dar es Salaam leo, ikiwa ni sehemu ya fedha zilizopatikana katika matamasha mbalimbali ya muziki wa Injili yaliyoandaliwa na kampuni hiyo. Kulia ni Mkurugenzi wa kituo hicho, Halima Ramadhan.
Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari, wakati alipokuwa akikabidhi kwa vituo vya kulelea yatima sehemu ya bidhaa za vyakula, mafuta, sabuni za kufulia, dawa za miswaki na mafuta ya kupakaa, Dar es Salaam leo, ikiwa ni sehemu ya fedha zilizopatikana katika matamasha mbalimbali ya muziki wa Injili yaliyoandaliwa na kampuni hiyo. Aliyembeba ni yatima Heida Edward (5) wa kituo cha Tuwakomboe.
Fredy Mwanjala, (TUDARCO)
VITUO 10 vya kulea watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu vya Dar es Salaam vimepatiwa msaada wa vyakula na vifaa vingine na kampuni ya Msama Promotions ambayo huandaa matamasha ya Krismasi, Pasaka na mengine ya muziki wa Injili.
Msaada huo umetolewa leo katika ofisi za kampuni hiyo zilizoko Kindondoni Dar es Salaam na Mkurugenzi wa wake Alex, Msama ambaye alisema ameutoa kwa sehemu ya mapato yaliyotokana na matamasha ya muziki wa Injili ambayo kampuni yake iliandaa.
Alisema ametoa msaada huo ikiwa ni utekelezaji wa moja ya mipango yake kusaidia jamii ya watu wenye uhitaji kama watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, wajane na wazee.
Alisema vyakula na vifaa vingine vya matumizi alivyotoa kwa vituo hivyo vina thamani ya sh.milioni 7.5.
"Msaada huu tumeutoa kutokana na matamasha tunayoyafanya, mapato tunayoyapata sehemu yake tumeichukua na kuwasaidia watoto yatima ili na wao wajione kuna watu wanaowajali. Leo tumetoa msaada huu ambao unathamani ya takribani shilingi milioni saba na nusu kwa ajili ya watoto yatima hawa," alisema Msama ambaye kampuni yake imeandaa tamasha la kumshukuru litakalofanyika Siku ya Krismasi Desemba 25, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Bidhaa zilizotolewa katika msaada huo ni pamoja na mchele, unga wa sembe, unga wa ngano, mifuko ya viroba ya sabuni za unga, sabuni za vipande, mafuta ya kupikia, mafuta ya kupakaa mwilini, dawa za meno na vingine.
Akizungumza baada ya kupokea msaada wa kituo chake, Mkurugenzi wa Kituo cha Honorata kilichoko Temeke, Honorata Michael ambaye ni mwenye ulemavu alisema anamshukuru Msama kutoa msaada wa vyakula na vifaa vingine vya matumizi kwa ajili ya kitu chake chenye watoto 82.
Alisema Msama amekuwa akitoa msaada kwa kitu chake na vingine kwa mwaka wa tatu mfululizo na kuzitaka kampuni,taasisi na watu wengine wenye uwezo kuwakumbuka watoto wanaishi kwenye mazingira magumu ambao wanahitaji kusaidiwa ili kuishi vizuri.
Naye Mwalimu wa Madrasa katika Kituo cha Rahman cha Magomeni, Hassan Ally alishukuru kwa kupatiwa msaada huo na kuwataka watu wengine kuwakumbuka watoto wanaoishi kwenye mzingira magumu ambao wamekusanywa kwenye vituo.
Vituo vilivyopata msaada huo na sehemu vilipo katika mabano ni Zaidia (Sinza),Hijar (Chang'ombe), Malaika (Kinondoni), Maunga Mkwajuni, Mwandaliwa (Boko), Sifa (Bunju) Honorata (Temeke), Chakuwawa ( Mwenge) na Rahman (Magomeni).

No comments:
Post a Comment