John Pombe Magufuli sasa ndiye rais mpya wa taifa la Tanzania baada ya kuapishwa rasmi kufuatia ushindi wake wa wingi wa kura katika uchaguzi mkuu uliopita.
Akiapishwa katika hafla iliohudhuriwa na viongozi mbalimbali,wakiwemo marais kutoka mataifa ya Afrika mashariki na kusini, Magufuli ameapa kutimiza ahadi zote alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Magufuli ambaye sasa ni rais wa awamu ya tano nchini Tanzania vilevile amewataka viongozi wa upinzani nchini humo kukubali kushindwa na kushirikiana naye katika juhudi zake za kuimarisha maisha ya taifa hilo.
Amesema kuwa licha ya kwamba alipata changomoto kubwa kutoka kwa upinzani alioupata amepata funzo kubwa kutoka kwao.
''Nashukuru wagombea wenzangu kwa kutupa changamoto,tumejifunza mengi kutoka kwao,lakini pia wajue kwamba uchaguzi umekwisha na rais ni John Pombe Magufuli'',alijigamba.
Awali aliyekuwa rais wa taifa hilo Jakaya Mrisho Kikwete aliwasili katika uwanja wa sherehe hiyo mbele ya umati mkubwa wa watu waliomkaribisha kwa vifijo na nderemo.
Kikwete aliuzunguka uwanja huo akiwapungia mkono wa kwaheri raia hao waliojaa uwanja huo.
Baadaye Bendera ya utawala wake ilishushwa huku rais mpya John Magufuli akiapishwa na makamu wake wa rais Samia Suluhu Hassan.
No comments:
Post a Comment