TANGAZO


Monday, November 30, 2015

Dola za Marekani Milioni 3.4 zatengwa kusaidia wachimbaji wadogo wa madini Tanzania

Mkuu wa Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu Serikali kutenga maeneo mbalimbali yenye ukumbwa wa ekari 197,432 kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchini. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa.(Picha na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)

Na Lilian Lundo – Maelezo
SERIKALI kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imetenga jumla ya Dola za Marekani Milioni 3.4 kusaidia vikundi vya wachimbaji wadogo na watoa huduma  katika migodi nchini.

Akiongea na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini Badra Masoud amesema, hatua hii imekuja baada ya  Serikali kubaini kwamba wachimbaji wengi wadogo huchimba madini kwa kutumia zana na vifaa duni kutokana na ukosefu wa  fedha za kununulia vifaa vya kisasa.

“Wachimbaji wadogo wengi hawawezi kukidhi masharti ya kupata mikopo katika benki za biashara nchini, hivyo Serikali inawajengea uwezo hatua kwa hatua hadi wafikie hatua ya kuweza kukopesheka katika mabenki ya kibiashara,” alisema Badra.

Aidha, Badra alisema kuwa pesa hizo zitatumika kwa miaka mitatu kuanzia mwaka huu wa fedha 2015/16 kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji madini wadogo kupata ruzuku kwa awamu ya tatu ili waweze kuchimba kisasa na kujiongezea vipato vyao na kuongeza pato la Taifa.

Badra alizidi kufafanua  kwa kusema kuwa, ruzuku hii ni jitihada za Serikali katika kukwamua wachimbaji wadogo kuondokana na umasikini kwa kuwajengea uwezo  wa kufikia  kuwa wachimbaji wa kati.

Vilevile Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, imetenga maeneo yenye ukubwa wa hekari 197,432 kwa ajili wa wachimbaji wadogo ili kuendeleza uchimbaji wa madini mdogo nchini.

Serikali itaendelea kuwa karibu na wachimbaji wadogo waliopatiwa ruzuku kuhakikisha fedha wanazopewa wanazitumia kama ilivyokusudiwa na si vinginevyo, wachimbaji hao watapewa elimu ya uchimbaji wa kisasa, utunzaji wa mazingira na namna ya kuepuka ajali ndani ya migodi.

No comments:

Post a Comment