TANGAZO


Wednesday, November 11, 2015

Diack ajiondoa kamati ya Olimpiki

Diack


Image copyrightGetty
Image captionDiack aliongoza IAAF miaka 16

Rais wa zamani wa shirikisho la riadha duniani IAAF Lamine Diack amejiuzulu kutoka kwa wadhifa wake kama mwanachama wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC.
Diack alikuwa tayari amesimamishwa kwa muda na IOC anapoendelea kuchunguzwa na maafisa wa polisi wa Ufaransa kwa tuhuma za kupokea hongo ili kuficha wanariadha waliogunduliwa wametumia dawa haramu alipokuwa uongozini IAAF.
Alikuwa tayari amejiuzulu kutoka kwa wakfu wa IAAF, ambao husimamiwa na IAAF.
Diack, 82, aliongoza IAAF kwa miaka 16.
Mnamo Jumatatu, IAAF ilihusishwa na tuhuma za kuchangia katika matumizi ya dawa za kusisimua misuli kwenye ripoti ya shirika la kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli duniani Wada.
Mwanawe Diack, Papa Massata, mshauri wake Habib Cisse na mkuu wa zamani wa kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli IAAF Gabriel Dolle pia wanachunguzwa na maafisa wa polisi wa Ufaransa.
Kwa mujibu wa viongozi wa mashtaka Ufaransa, Diack anashukiwa kupokea pesa kuahirisha adhabu dhidi ya wanariadha kadha wa Urusi waliopatikana na hatia ya kutumia dawa zilizoharamishwa 2011, kabla ya kuandaliwa kwa Michezo ya Olimpiki.
IOC ilisema Jumanne kuwa: "Bodi kuu tendaji adhuhuri hii imeamua kuidhinisha pendekezo la kamati ya kinidhamu ya IOC kumsimamisha Bw Lamine Diack, aliyekuwa rais wa IAAF, uanachama wake katika IOC."
Taarifa hiyo iliendelea kuhimiza IAAF kuchukua hatua dhidi ya wanariadha wa Olimpiki waliotajwa kwenye ripoti hiyo ya Wada.
Diack alifikisha kikomo uongozi wake wa miaka 16 katika IAAF mwezi Agosti, huku Mwingereza Coe, mshindi mara mbili wa Olimpiki mbio za 1500m, akichaguliwa kumrithi.

No comments:

Post a Comment