Chelsea walimpunguzia presha meneja wao Jose Mourinho baada ya bao la dakika za mwisho kutoka kwa Willian kuwapa ushindi muhimu wa 2-1 katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Dynamo Kiev uwanjani Stamford Bridge.
Mourinho amekuwa na masaibu mengi, baada ya klabu yake kuanza vibaya sana kampeni ya kutetea taji la Ligi ya Premia, kwa sasa wakiwa nambari 15 kwenye jedwali.
Ilionekana kana kwamba matatizo yao yangezidi baada ya Aleksandar Dragovic kufidia bao lake la kujifunga kwa kutumia vyema kosa la kipa Asmir Begovic na kufungia timu yake bao la kusawazisha mechi ikiwa imesalia dakika 13 kumalizika.
Mashabiki wa Chelsea, walioimba jina la Mourinho mechi yote, lazima waliingiza maji tumboni lakini Willian aliwaokoa kwa kombora kali alilolitoa akiwa hatua 25 kutoka kwenye goli dakika sita baadaye.
Ushindi huo ulifikisha Blues nambari mbili Kundi G, wakiwa alama tatu nyuma ya viongozi Porto lakini sasa wana pengo la alama mbili kati yao na Dynamo Kiev.
Mourinho alihitaji sana kitulizo na alikuwa na furaha mashabiki walimuunga mkono.
Isitoshe, familia yake – mkewe Matilde, bintiye Matilde Jr na mwanawe wa kiume Jose Jr - ilikuwepo uwanjani.
Mourinho sasa atatumai kuwa vijana wake wataweza kushinda mechi ya Jumamosi dhidi ya Stoke City, mechi ambayo hawezi kuhudhuria baada ya kupigwa marufuku mechi moja kwa utovu wa nidhamu.
Takwimu muhimu
- Chelsea sasa wameenda mechi sita Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya bila kushindwa nyumbani, wakishinda nne na kutoka sare mbili.
- Chelsea wamefaidika kutokana na mabao manne ya kujifunga katika mashindano yote msimu huu. Ni Willian pekee aliyewafungia zaidi (mabao matano).
- Aleksandar Dragovic ndiye mchezaji wa 11 Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kujifunga na pia kufungia timu yake katika mechi moja.
No comments:
Post a Comment