TANGAZO


Wednesday, November 11, 2015

Balozi Seif Iddi akagua jengo la Beit Al – Ajaib lililoporomoka paa kutokana na upepo mkali Mjini Unguja

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani akimfafanulia jambo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  wakati wakikagua athari iliyopelekea Paa la Jumba la Wananchi Forodhani kuanguka kutokana na upepo mkali uliovuma ghafla. Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Mh. Ramadhan Abdulla Shaabad na kushoto ya Balozi ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Nd. Ali Khalid Mirza.
Sehemu ya juu ya Paa la Jumba la Kihistoria liliopo  Forodhani ikionekana kubomoka kufuatioa upepo Mkali uliovuma ghafla lakini haukuathiri maisha ya wapiti njia.
Muonekano wa juu wa Jumba la Kumbukumbu ya Kihistoria Forodhani { Beit Al-Ajaib } ambao unaonyesha kuathirika kutokana na kubomoka kwa mara mbili mwaka 2013 na mwaka huu kutokana na kukumbwa na upepo mkali wa msimu wa Mvua za Vuli. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
11/11/2015.
UPEPO mkali uliovuma ghafla jana  mchana umesababisha kuporomoka kwa paa upande wa  Magharibi la Jumba la Makumbusho  ya Taifa Zanzibar (Beit Al – Ajaib), liliopo pembezoni mwa Fukwe ya Bahari ya Hindi Forodhani Mjini Zanzibar.

Mporomko huo wa Paa hilo pia ulizikumba Gari Tatu zilizokuwa zimeegeshwa pembezoni mwa Jumba hilo ambazo mbili kati yake zilipata athari ya michubuko midogo midogo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Karani alieleza hayo wakati akitoa ufafanuzi mbele ya  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika eneo hilo kuangalia hali halisi ya tukio hilo lililoleta mshituko kwa wakaazi pamoja na wapiti njia katika  eneo hilo.

Nd. Sarboko alisema upepo unaokuwa ukivuma katika vipindi vya Majira ya Msimu wa Mvua za Vuli  tayari umeshawahi kuathiri Jumba hilo mwaka 2013 na kusababisha kuvunjika  katika sehemu ya juu nyuma ya jengo hilo la Kihistoria.

Alisema athari hiyo ilitoa fursa   kwa Serikali ya Oman kupitia Ubalozi wake Nchini Tanzania kuonyesha nia ya kutaka kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kulifanyia matengenezo makubwa Jumba hilo.

“ Matayarisho ya matengenezo makubwa ya jumba la Makumbusho ya Taifa (Beit Al – ajaib),  Forodhani yalianza tokea lilipoporomoka  mwanzo mwaka 2013 ”. Alisema Nd. Issa  Sarboko Makarani.

Alieleza kwamba taratibu za awali ukiwemo ushauri wa Shirika la Elimu, Sayansi   na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) zilichukuliwa  ikizingatiwa kwamba Mji Mkongwe wa Zanzibar ni miongoni mwa Miji iliyobahatika kuwemo ndani ya Urithi wa Kimataifa.

Mkurugenzi huyo wa Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar alifahamisha kuwa kinachosubiriwa kwa sasa ni Serikali ya Oman kutoa Tenda kwa  ajili ya kumteua Mkandarasi atakayehusika kulifanyia matengenezo makubwa Jumba hilo.

Alisema matengenezo ya Jumba hilo yatazingatia zaidi umbile lake lile lile lililokuwepo katika ramani yake ya mwanzo tokea lilipojengwa mnamo   mwaka 1883 ambayo itaendelea kuwa kiashiria cha nembo ya Mji wa Zanzibar.

“ Jumba hili la ajabu katika kuzingatia masharti ya Unesco ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe kupitia Urithi wa Kimataifa litafanyiwa matengenezo katika umbile lake lile lile la mwanzo ili kuikabisha haiba ya eneo hilo muhimu kwa Historia na Utalii Duniani ”. AlisemaMkurugenzi Sarboko.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi alielezea faraja yake kutokana na juhudi  kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe wa Zanzibar katika kusimamia haiba halisi ya eneo hilo.

Mji Mkongwe wa Zanzibar ni miongoni mwa Miji michache Duniani iliyopata bahati ya kuteuliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni  la Umoja wa Mtaifa (Unesco) kuwa urithi wa Kimataifa.

No comments:

Post a Comment