Mgeni rasmi katika mahafali ya 13 ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Shimbwe iliyopo Uru wilayani Moshi vijijini, Ofisa Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Georgia Mutagahywa akimtunuku cheti Loth Rajabu ambaye ni mmoja wa wahitimu katika shule hiyo.
Mgeni rasmi katika mahafali ya 13 ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Shimbwe iliyopo Uru wilayani Moshi vijijini, Ofisa Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Georgia Mutagahywa akimtunuku cheti Christina Lyimo ambaye ni mmoja wa wahitimu katika shule hiyo.
Mgeni rasmi wa mahafali ya 13 ya shule ya sekondari Shimbwe iliyopo Moshi vijijini, Ofisa Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, Georgia Mutagahywa (kushoto) akiongozana na mkuu wa shule ya sekondari hiyo, Jacob Costantine kuelekea katika jukwaa wakati wa mahafali hiyo ya kidato cha nne katika shule hiyo.
Mgeni rasmi katika mahafali ya 13 ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Shimbwe iliyopo Uru wilayani Moshi vijijini, Ofisa Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Georgia Mutagahywa akitoa hotuba yake katika mahafali hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki shuleni hapo.
Na Mwandishi wetu
KUNA umuhimu na haja ya watoto wetu wanaojua kusoma na kuandika na walio na upeo mzuri kielimu na maadili mazuri ya kifamilia kutokubaki nyuma ya teknolojia kwa karne hii ya 21. Hayo yalibainishwa na mgeni rasmi wa mahafali ya 13 ya kidato cha Nne katika shule ya Shimbwe iliyopo Uru Moshi vijijini.
Akizungumza katika mahafali hiyo akiwa ndiye mgeni rasmi Ofisa Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,Georgia Mutagahywa, aliyekuwa ameongozana na Mwenyekiti wa Hassan Majaar Trust (HMT) Balozi Mwanaidi Majaar alisema kampuni ya Vodacom Tanzania inatarajia kuleta wataalamu kutoka Learning In Sync kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo.
“Teknolojia ndio mkombozi na ndio sababu sisi tunasema hakuna mtoto atakayebaki nyuma katika teknolojia,siku za karibuni watakuja wataalamu ambao ni wadau wetu wakubwa katika masuala ya teknolojia ambao wataweza ku train(toa mafunzo) waalimu na wanafunzi katika programu mbalimbali kwa kutumia silabasi za kitanzania.”alisema Mutagahywa.
Pia aliendelea kusema kuwa kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania kupitia mfuko wake wa kusaidia jamii”Vodacom Foundation” imepanga kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la T-MARC Tanzania kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Shimbwe juu ya kubadili maisha ya watoto, kimalezi na kimakuzi.
Hatua ya Vodacom foundation kuchukua jukumu hilo inatokana na taarifa ya baadhi ya watoto wa kike katika shule hiyo kushindwa kumaliza masomo yao ya sekondari kutokana na kubeba ujauzito wakiwa shuleni.
Akiendelea kuzungumza katika mahafali hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki ,Ofisa huyo aliyekuwa mgeni rasmi, alisema Vodacom kwa kutambua changamoto hiyo imepanga kutoa nyenzo kwa watoto wa kike.
“Hili suala la Mimba za utotoni tuna wadau wanaofanya kazi na watoto wa kike na tunatambua changamoto za mtoto wa kike,lakini tunataka kuwapa nyenzo za kuwawezesha kuvuka na mnaweza kuvuka na mkawa wanawake wa maana katika uongozi wa nchi”alisema Mutagahywa.
“Ni lazima tufike mahali ambapo watoto wetu wa kike na kiume tuone wanaweza kuheshimiana na kusaidiana ili taifa liweze kusonga mbele …Hata ukipata mimba ukisha jifungua rudi shule ukasome,ukianguka unanyanyuka na unaendelea…..kwa hiyo nitazungumza na wadau wetu T-MARC waje wazungumze na wasichana na wavulana kuhusu suala la mimba kwa sababu si mimba zote zinatoka kwa fataki.”aliongeza Mutagahywa.
Kwa upande wake Balozi Majaar alitoa pongezi kwa kampuni hiyo na wanafunzi wa kidato cha Nne na kuwatakia kila la heri katika mitiani yao ijayo na pia alimpongeza Ofisa huyo wa Vodacom Tanzania kwa kuendelea kusaidia jamii ya watanzania hasa katika eneo la Elimu ambalo limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za madawati.
“Niwashukuru sana Vodacom Tanzania,hasa mgeni rasmi ni mwanamke ambaye yeye muombe chochote hasa kwenye masuala ya elimu ,atajitolea na wakati mwingine huchangisha wafanyakazi wenzake ili pesa zipatikane kuchangia shule, tulivyomuomba hakusita kwa vile tayari aliwahi kuja shimbwe kuangalia juu ya masuala ya kompyuta”alisema Balozi Majaar.
Awali akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi mkuu wa shule ya sekondari Shimbwe, Jakob Costantine alisema shule yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya nyumba za walimu hali inayowalazimu kuishi mbali na ilipo shule hiyo.
“Ombi letu kwa serikali itusaidie upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa majengo ya shule na nyumba za walimu na upatikanaji wa tanki kubwa kwa ajili ya kuhifadhia chakula”alisema Costantine.
Mbali na Ombi hilo, Mkuu huyo wa shule pia aliomba kujengwa wa mnara kwa ajili ya mawasiliano ya simu katika maeneo ya jirani na shule ili kuwezesha upatikanaji wa urahisi wa mawasiliano pamoja na kurahisisha mafunzo ya kompyuta shuleni hapo.






No comments:
Post a Comment