Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Kilimani Kidoti wakisikiliza
nasaha za Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif baada ya kumueleza changamoto wanazopambana
nazo kijijini kwao.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwaahidi Wananchi wa Kijiji cha Kilimani Kidoti
kwamba Serikali Kuu itazingatia changamoto zinazowakabili na kuzifanyia kazi
inayostahiki. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
14/10/2015.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi ameahidi kufutilia na hatimae Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutafuta mbinu za kutanzua changamoto zinazowakabili
Wananchi wa Shehia ya Kilimani Kidoti Jimbo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema changamoto hizo zikiwemo fidia ya nyumba,
mazao, Madrasa pamoja na uvamizi wa eneo la Ardhi zitapatiwa ufumbuzi bila ya
kuleta hitilafu kwa upande wowote uliohusika na changamoto hizo.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa ahadi hiyo wakati
akizungumza na Wananchi wa Shehia ya Kilimani Kidoti mara baada ya kupokea kero
zinazowakabili ambazo nyengine zina muda mrefu sasa bila ya kupatiwa ufumbuzi
Mkutano uliofanyika katika Skuli ya Maandalizi ya Kilimani Kidoto Jimbo la
Nungwi.
Alisema Mwananchi wote wa Taifa hili wanahitaji
kupata maendeleo katika maeneo
wanayoishi kwa vile maendeleo hayo hayana itikadi, kabila, rangi, dini wana
sehemu wanayotoka.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inalielewa tatizo la Wananchi hao kuhusu fidia za mali na mazao
yao kufuatia kupita kwa Bomba ya huduma za maji safi na salama katika Kijiji
chao.
Alisema juhudi
zitachukuliwa na Serikali Kuu kupitia Wizara ya Fedha kulipa fidia ya mali na mazao ya Wananchi hao
kadri hali itakavyoruhusu kwa lengo la kuwaondoshea usumbufu Wana Kijiji hao
hasa wale waliobomolewa nyumba zao.
Akizungumzia suala la Maskani ya CCM ya Kijiji hicho
iliyohodhiwa na upande wa Upinzani Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati
Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi aliwanasihi Wana CCM wa
Kijiji hicho kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa Jengo jengine.
Alisema yeye binafsi atakuwa tayari kusaidia nguvu
za uwezeshaji wa Vifaa kwa ajili ya ujenzi huo hatua ambayo itaondosha fitna,
majungu na mgongano unaoweza kuleta athari hapo baadaye baina yao na wale wa
Upinzani walioamuwa kuihodhi maskani yao.
Naye Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama
Asha Suleiman Iddi aliwataka Wananchi wa Kijiji hicho kuwa na subra huku
akitafuta nguvu za ufadhili ili kuanza kuunga mkono ujenzi wa Madrasa ya Kijiji
hicho.
Mama Asha alisema
hatua zitachukuliwa katika kutoa vifaa vitakavyoanzia ujenzi huo ili
kutekeleza ahadi iliyotolewa kwa Wana Kijiji hao kusaidiwa nguvu za ujenzi huo.
Wakitoa
changamoto zinazowakabili baadhi ya
Wawakilishi wa Wananchi hao walilalamikia lugha za Ubabe zinazotolewa
dhidi yao kutoka kwa baadhi ya Viongozi wanaoteuliwa na Serikali.
Walisema licha ya jitihada wanazoendelea kuchuku za
kufuatilia changamoto wanazopambana nazo katika ngazi mbali mbali kuanzia
shehia hadi Mkoa lakini bado wamekuwa wakipambana na lugha mbovu zisizostahiki
kutolewa na Viongozi hao.



No comments:
Post a Comment