*Bingwa shirikisho kulamba sh. mil 50
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (katikati) akizungumza wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa udhamini mashindano ya Kombe la Shirikisho, litakalofahamika kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), Dar es Salaam leo. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Rhys Torrington na kushoto ni Makamu wa Rais wa Klabu ya Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu'. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (katikati) akizungumza wakati wa hafla hiyo, ya kusaini mkataba wa udhamini mashindano ya Kombe la Shirikisho, litakalofahamika kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), Dar es Salaam leo.
Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Rhys Torrington (kulia), akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo, wa udhamini mashindano ya Kombe la Shirikisho litakalofahamika kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), Dar es Salaam leo.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Rhys Torrington (kulia), wakisaini mkataba wa udhamini mashindano ya Kombe la Shirikisho litakalofahamika kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), Dar es Salaam leo. Kulia aliyesimama ni Makamu wa Rais wa Klabu ya Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' na kushoto ni Ofisa Masoko wa TFF, Peter Simon.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Rhys Torrington (kulia), wakibadilishana hati za makataba huo, mara baada ya kuusaini, mkataba unaohusu udhamini mashindano ya Kombe la Shirikisho litakalofahamika kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), Dar es Salaam leo.
Kiongozi wa timu ya Friends Rangers moja ya timu zitakazoshiriki kombe hilo, Elly, akizungumza katika hafla hiyo.
Ofisa Masoko wa TFF, Peter Simon, akitangaza timu mwenyeji na wageni katika hatua za mwanzo za mashindano ya kombe hilo.
Viongozi wa TFF na Azam Media wakipiga picha ya pamoja mara baada ya kusaini mkataba huo, jijini leo.
Na Mwandishi wetu
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa udhamini wa Kampuni ya Azam Media kupitia Azamtv Sports, limezindua Kombe la Shirikisho litakalofahamika kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) ambalo litaanza kutimua vumbi Novemba mwaka huu kwa kushirikisha timu 64, huku bingwa akiondoka na zawadi ya sh. milioni 50.
Michuano hiyo imerejeshwa baada ya kukosekana kwa takribani miaka 13, ambapo kwa utaratibu mpya bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAFCC).
Rais wa TFF, Jamal Malinzi akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa michuano hiyo, Dar es Salaam leo ambapo pia ilitajwa ratiba ya awali, aliishukuru Azam Media, iliyowakilishwa na Mkurugenzi wake, Rhys Thorrington kwa kudhamini michuano hiyo, hali ambayo itaongeza ushindani zaidi nchini.
Malinzi alizitaka klabu zitakazoshiriki michuano hiyo, kuonesha ushindani ikiwa ni nafasi pekee ya kuitangaza na kuonekana kuwa itakuwa ikioneshwa moja moja na runinga ya Azamtv.
Alisema kila timu inayoshiriki michuano hiyo itapata fedha ya usafiri sh.milioni 3, na vifaa vitakavyotolewa na mdhamini kampuni ya Azam Media.
Naye Mkurugenzi wa Azam media, Rhys Thorrington alisema udhamini huo wa miaka minne una thamani ya fedha za Tanzania sh. bilioni 3.3, timu shiriki zitapata nafasi ya kuonekana moja moja katika nchi zaidi ya saba barani Afrika kupitia Azamtv.
Mshindi wa Kombe la ASFC linalodhaminiwa na kampuni ya Azam kupitia Azamtv Sports, atajinyakuliwa kitita cha sh. milioni 50, jumla ya timu 64 kutoka Ligi Kuu (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) zitashiriki michuano hiyo.
Alizitaja timu hizo ni 24 za ligi daraja la pili na 8 za Ligi Daraja la Kwanza 3, zilizopanda daraja na 5 zilizoshika nafasi za chini kwenye makundi yote zitashiriki katika mzunguko wa kwanza Novemba kwa kucheza mechi 16 na kupata washindi 16 ambao wataingia raundi ya pili.
Timu 16 zilizoshinda raundi ya kwanza na 16 zilizofanya vizuri Ligi Daraja la Kwanza zitachanganywa na kupangwa kucheza mechi 16 nyingine za mzunguko wa pili Desemba mwaka huu .
Washindi wa raundi ya pili wataingia mzunguko wa tatu, watachanganywa na timu 16 za Ligi Kuu na kuchezwa mechi 16, washindi wake wataingia raundi ya nne, mzunguko huo wa tatu itafanyika Januari 2016.
Timu 16 zilizoshinda mzunguko wa tatu zitaingia raundi ya nne ambayo itakuwa na mechi 8 na washindi 8 wataingia raundi ya tano au robo fainali Februari 2016.
Baada ya kufanyika droo, robo fainali itachezwa Machi 2016, washindi watapangwa kucheza nusu fainali au raundi ya 6 Aprili.
Washindi wa nusu fainali watapambana katika fainali na kumpata bingwa wa Azam Sports Federation Cup 2015/16. Mechi ya fainali itachezwa wiki moja baada ya Ligi Kuu kumalizika na bingwa atakabidhiwa kombe na zawadi ya fedha tasilimu sh.milioni 50.
Mechi za mzunguko wa kwanza na wa pili kama mshindi hatapatikana ndani ya dakika 90 itatumika sheria ya kupigiana penalti moja kwa moja. Mechi za mzunguko wa tatu na wa nne, kama mshindi hatapatikana ndani ya dakika 90 mechi itarudiwa katika uwanja wa timu iliyokuwa mgeni mechi ya awali.
Mechi za robo fainali au raundi ya tano kama mshindi hatapatikana ndani ya dakika 90 hatua ya penalti tano tano itaamua mshindi.
Kwa mechi za nusu fainali na fainali kama mechi itaisha kwa sare ndani ya dakika 90, dakika 30 za nyongeza zitachezwa, na kama hakutakuwa na mshindi penalti zitaamua mshindi.

No comments:
Post a Comment