TANGAZO


Sunday, September 27, 2015

Rais Kikwete mgeni rasmi Tamasha la Kuombea Amani, Uchaguzi Mkuu Oktoba 4, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandali ya Tamasha la kuiombea Nchi amani na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, litakalofanyika Oktoba 4, mwaka huu, Alex Msama akifafanua jambo kwa waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, wakati alipomtangaza Mgeni rasmi wa tamasha hilo, Rais Jakaya Kikwete. Tamasha hilo, litafanyika Uwanja wa Taifa jijini. Kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Hamisi Pembe. (Picha na Loveness Bernard)
  
Na Mwandishi wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha  maalumu la kuombea nchi amani na Uchaguzi Mkuu, litakalofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Oktoba 4.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati inayoratibu tamasha hilo, Alex Msama alisema ni faraja kubwa kwao, kuona Rais anakubali mwaliko wao wa kuwa mgeni rasmi.

“Tumefurahi sana kuona Rais wa nchi anakubali kuwa mgeni rasmi katika tukio hilo la kuombea amani, Uchaguzi Mkuu kwa manufaa ya taifa letu, sisi tukiwa waratibu wa tukio hili tumefarijika mno,” alisema Msama.

Alisema tukio hilo litakalowaleta pamoja viongozi wa kada zote wakiwamo wale wa madhehebu na dini mbalimbali bila ubaguzi, litasindikizwa na burudabi ya nyimbo za injili kutoka kwa waimbaji wa ndani na nje ya nchi.

Msama alisema Kamati ya maandalizi iliamua kumuomba Rais Kikwete sio tu kwa kutambua nafasi yake katika taifa, pia moyo wake wa kuhimiza amani wakati wote wa utawala wake ikiwemo kushiriki matamsha ya injili.

Alisema, mbali ya kuwaongoza Watanzania kuombea taifa lao lipite salama katika uchaguzi mkuu, pia wadau wa muziki wa injili watalitumia tukio hilo kumuga na kumshukuru kwa mchango wake katika kukuza muziki wa injili.

Akifafanua nafasi ya Rais Kikwete kukuza muziki huo, Msama alisema katika harakati zake za kuratibu matukio ya muziki wa injili, kiongozi huyo amewahi kuwa mgeni rasmi katika tamasha la Pasaka mwaka 2011.

Msama alisema kitendo cha Kikwete kutokuwa mbaguzi wa dini, ndio maana Kamati ya kuratibu Tamasha la kuombea Amani Uchaguzi Mkuu imempa heshima kutokana na kuwa kielelezo cha amani na mshikamano.

Alisema ujumbe mahususi katika Tamasha hilo ni kwamba, suala la amani na utulivu, ni jukumu la kila mmoja kwa nafasi yake kwani thamani ya tunu ya amani haiwezi kuonekana kwa wepesi hadi pale inapotoweka.

Msama alisema Kamati yake imejitwisha jukumu hilo la kuhimiza amani katika uchaguzi mkuu kutokana na kuwepo kwa viashiria vya uvunjivu wa hiyo amani kutokana ushindani mkali uliopo katika uchaguzi wa safari hii.

Ushindani mkali katika uchaguzi huo umetuama kati ya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa anayeungwa mkono na vyama vinne ninavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Dk. John Magufuli wa CCM.

Msama alisema, baada ya uzinduzi kufanyika Uwanja wa Taifa siku hiyo ambapo kiingilio kitakuwa sh 5000; 3000 kwa wakubwa na sh 1,000 kwa watoto, tamasha hilo litaelekea katika mikoa 10 kuhamasisha amani.

Miongoni mwa waimbaji wa kigeni waliothibitisha kushiriki na nchi zao kwenye mabano ni Solly Mahlangu na Sipho Makhabane (Afrika Kusini), Ephraem Sekereti (Zambia), Anastazia Mukabwa na Solomon Mukubwa Kenya.

No comments:

Post a Comment