Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw.Raymond Mapunda akitoa matokeo ya mtihani wa Utimilifu kwa wanafunzi wa shule za Sekondari jijini Dar es salaam ambapo katika mtihani huo uliofanyika Mei 25 hadi Juni 12 mwaka huu shule Binafsi zimeongoza kwa ufaulu. (Picha na Aron Msigwa)
Na Aron Msigwa -MAELEZO.
5/8/2015.Dar es salaam.
MATOKEO ya mtihani wa Utimilifu kwa wanafunzi wanaosoma kidato cha nne katika shule za Sekondari za jiji la Dare es Salaam yametolewa leo jijini Dar es Salaam yakiwa na alama za juu za ufaulu kwa wanafunzi wanaosoma Katika shule zisizomilikiwa na Serikali.
Akitoa matokeo hayo, Afisa Elimu wa Mkoa huo Bw. Raymond Mapunda amesema kuwa ufaulu mzuri umeonekana zaidi katika shule Binafsi kuliko za serikali kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanywa na walimu wa shule hizo.
Amesema kuwa licha ya mkoa wake kuwa na idadi ya walimu wa kutosha katika shule zinazomilikiwa na Serikali bado wanafunzi wa kidato cha nne wa shule hizo wamefanya vibaya ikilinganishwa na wale wanaosoma shule binafsi.
Amesema mtihani huo ulifanyika Mei 25 hadi Juni 12,2015 mwaka huu na ulihusisha shule 292 na kuongeza kuwa wanafunzi wapatao 40,356 walisajiliwa kufanya mtihani huo.
Bw.Mapunda amesema kati ya hao 39,480 ambao ni sawa na asilimia 97.8 walifanya mtihani huo huku 876 ambao ni sawa na asilimia 2.2 walishindwa kufanya mtihani huo kutokana na sababu za ugonjwa na utoro.
Ameeleza kuwa kutokana na idadi iliyosajiliwa, wanafunzi 37,560 wamefaulu mtihani huo kulingana na madaraja mbalimbali yaliyoainishwa, huku idadi kubwa ya wanafunzi wapatao 26,265 imeangukia katika daraja la mwisho la ufaulu.
"Uchambuzi wa kina tulioufanya umeonesha shule za Serikali zilizo nyingi zinazochukua wanafunzi 28,273 hazikufanya vizuri ikilinganishwa na shule Zisizo za Serikali zenye idadi ya wanafunzi 11,207 hivyo Maafisa wa Elimu wa Manispaa waendelee kufuatilia kwa karibu hali hii" Amesisitiza.
Aidha, amezitaja shule kumi bora za Serikali zilizofanya vizuri kimkoa katika mtihani huo kuwa ni pamoja na Jangwani,Pugu,Kisutu,Zanaki,Chang'ombe,Azania,Dar es salaam,KIbasila,Ilala na Benjamin Mkapa.
Kwa upande wa Binafsi amesema ni pamoja Main Green Hill,Canossa ambayo imeshika nafasi 5 mfululizo ikifuatiwa na Feza Boys nafasi 3 mfululizo na shule ya Sekondari Alpha.
Ameongeza kuwa katika matokeo matokeo ya shule zote wasichana wameongoza kwa kuwa na ufaulu wa juu kuliko wavulana.
"Napenda kuwafahamisha wananchi wa mkoa wa Dar es salaam kuwa matokeo haya yanaendelea kuchambuliwa kimasomo na kwa gredi na uchambuzi wote utawekwa kwenye tovuti ya Mkoa wa Dar es salaam ya www.dsm.go.tz ili kilia mdau ,shule,mwalimu na mwanafunzi aweze kuyatumia.
No comments:
Post a Comment