TANGAZO


Saturday, August 8, 2015

Klabu ipi maarufu zaidi Afrika ligi ya England?

Mshirikishe mwenzako

Mashabiki wa Ligi Kuu England barani Afrika

Kwa mashabiki wa soka barani Afrika, Ligi Kuu ya England ndio sasa basi, ndio mwisho wa kila kitu, ndio eneo lao la maabadi. Nembo hii ya kimataifa katika soka inafuatiliwa na zaidi ya watu bilioni moja kote duniani na watu milioni 260 kati ya hao wapo barani Afrika.
Huku msimu mpya wa mwaka 2015-16 ukianza, majumba ya starehe na mikahawa kutoka Cape Town hadi Cairo itakuwa ikijiandaa kukidhi mahitaji ya mashabiki wengi watakaokuwa wakifika tayari kushudia kipute hicho kwenye runinga kubwa kubwa zilizotundikwa ukutani.
Lakini ni timu gani ambayo ni maarufu zaidi katika bara hili?
Huenda tusiweze kabisa kujibu swali hili kikamilifu, japo utafiti uliofanywa na twitter unatupa sura ya wastan, kwa kukadiria idadi ya jumla ya watu katika kila taifa ambao wanafuata anwani rasmi ya timu za ligi kuu England kwenye twitter na kisha kuziainisha tarakimu hizo katika asilimia kwa kila kilabu.
Magharibi


Hapana shaka Chelsea ndio maarufu zaidi katika eneo hili. Hutoweza kuzungumzia Ligi kuu nchini Englan katika eneo la Magharibi mwa Afrika bila kuwazia Didier Drogba, Solomon Kalou, Samuel Eto'o, Victor Moses, Michael Essien na John Mikel Obi, wote ni wenyeji wa Afrika ya Magharibi ambao wameichezea The Blues.
Hata hivyo, Drogba ndiye mashuhuri zaidi kutokana na mafanikio yake nje na ndani ya uwanja. Hapana shaka kwamba alikuwa mshambulizi mtajika klatika klabu hiyo, akifunga bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti na kuisaidia Chelsea kunyakuwa taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2012, na pia kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika Magharibi kufunga jumla ya mabao 100 katika Ligi kuu England mwaka huo.
Kadhalika Drogba anaheshimika sana nyumbani Ivory Coast kwa juhudi zake za kueneza amani baada ya mzozo ulioibuka kati ya mwaka 2010-2011, na ameanzisha wakfu wake kuimarisha afya na elimu katika taifa hilo.
Mashariki


Chaguo la wengi katika eneo la Afrika Mashariki ni rangi nyekundu ya Arsenal. Umaarufu mkubwa zaidi wa the Gunners katika eneo hili unaweza kuwa ulitokana na dhana ya kuwa timu 'isiyoweza kushindwa', baada ya timu hiyo kuvunja rekodi katika msimu wa mwaka 2003-04 kwa kunyakuwa ligi bila kupoteza mechi yoyote, ilicheza mechi 49 bila kupoteza yoyote.
Mafanikio ya wachezaji wa Kiafrika kama vile Nwankwo Kanu, Emmanuel Adebayor, Kolo Toure na Lauren ilifanya Arsenal kuwa maarufu hata zaidi. Kanu bila shaka ndiye sababu ya Arsenal kupata umaarufu mkubwa nchini Nigeria.
Jambo la kushangaza ni kwamba Afrika Mashariki imepata kutuma mchezaji mmoja pekee katika Ligi Kuu nchini England - mchezaji wa timu ya taifa ya Kenya na kilabu ya Southampton Victor Wanyama.
Kusini


Sio jambo la kushangaza kuwa Manchester United ndio timu mashuhuri zaidi katika eneo la kusini mwa Afrika.
Manchester United ndio timu yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Ligi Kuu England, baada ya kushinda jumla ya mataji 13 tangu ligi hiyo ianze mwaka 1992.
Pia Manchester United iliwahi kumsajili mmoja wa wachezaji mashuhuri zaidi wa Afrika Kusini, Quinton Fortune, aliyewachezea Red Devils kwa kipindi cha miaka saba.
Fortune pia ni mmoja wa wachezaji wengi wa zamani wa Man U wanaozuru eneo hilo kila mwaka kutangaza timu hiyo. Afrika kusini ilikuwa nchini ya kwanza barani Afrika kuwa na chama cha wapambe wa Manchester United.
Kaskazini


Kwa watu wa Afrika Kaskazini Arsenal ndio timu maarufu zaidi. The Gunners inawakilishwa vilivyo nchini Morocco, Algeria na Tunisia.
Vyama vya wapambe wa klabu hiyo katika mataifa haya vimesaidia kuipa klabu hiyo umaarufu kupitia mashindano kama vile mbio za kila mwaka za "Be a Gunner. Be a Runner".
Lakini nchini Misri, ni Chelsea ndio inayotawala - hii ni baada ya timu hiyo kumnunua Mohamed Salah kwa kima cha dola $17m aupauni £11m mwezi Januari mwaka 2014.
Timu za Ligi Kuu England zenye ufuasi mkubwa zaidi kwenye Twitter:
@Arsenal - wafuasi milioni 6.14
@ChelseaFC - wafuasi milioni 5.92
@ManUtd - wafuasi milioni 5.73
@LFC - wafuasi milioni 4.64
@MCFC -wafuasi milioni 2.59
Shiriki:
Ni timu ipi unayounga mkono? Uliamua vipi kuwa mfuasi wa timu yako? Ni wakati gani umejikuta ukiwa ''shabiki sugu'' katika Ligi Kuu nchini England? Tutumie majibu yako kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi au ukanda wa video kwa kuambatanisha neno lenye alama ya reli #EPLStories kwenye Twitter. Tutasambaza baadhi ya jumbe hizi kwenye anwani ya @bbcswahili.
Au wasiliana nasi kwenye ukurasa wetu wa Facebook BBCSwahili kushiriki mjadala kabla ya kuanza kwa kipute cha Ligi Kuu nchini England siku ya Jumamosi.

No comments:

Post a Comment