Mwenyekiti mpya wa Mashindano ya Miss Tanzania, Juma Pinto akiongea na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni msemaji wa kamati hiyo, Miss Tanzania namba 2 mwaka 2006 Jokate Mwegelo. (Picha na Maelezo)
Allen Mhina Na Ally Daud – Maelezo
27/8/2015.Dar es Salaam.
KAMATI inayosimamia mashindano ya Miss Tanzania Lino International Agency imepata Mwenyekiti na wajumbe wapya watakaoandaa ,kuratibu na kusimamia mashindano ya urembo ya Miss Tanzania.
Akiwatambulisha wajumbe hao mbele ya waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam, aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati ya Miss Tanzania iliyomaliza muda wake Hashim Lundenga amesema kuwa kamati mpya ndiyo itakayowajibika na shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na kamati ya awali.
Amesema kamati hiyo itafanya kazi zake kwa kuzingatia sheria na vigezo vyote vya kimaadili ili kuepuka ukiukwaji wa taratibu za mashindano hayo.
“Hatutamvumilia mwanakamati yeyote atakayevunja miiko ya mashindano haya, sisi tutakuwa nyuma tukiangalia kwa umakini”, amesema Bw. Lundenga.
Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa kamati hiyo Juma Pinto ametoa pongezi za dhati kwa kamati iliyomaliza muda wake na kuhaidi kukubaliana na mfumo unatumika kuratibu mashindano hayo .
“Namshukuru Lundenga kwa kunikabidhi nafasi hii ya mwenyekiti wa kamati ya miss Tanzania, naahidi kuratibu mashindano haya kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa ili kamati yangu iweze kukidhi haja ya mashindano haya”. Amesema.
Naye Msemaji Mkuu wa kamati hiyo na aliyekuwa Miss Tanzania namba mbili mwaka 2006 Jokate Mwegelo, ametoa rai kwa wasichana wa kitanzania wajitokeze kushiriki mashindano hayo kwa kuonesha vipaji walivyonavyo na kupata ajira.
Mwishoni mwa mwaka jana Mashindano ya Miss Tanzania yalikumbwa na mtafaruku wa ukiukwaji wa maadili na vigezo vya mashindano na kulazimika kusimamishwa kwa muda na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA).
No comments:
Post a Comment