Naibu Meneja Masuala ya Kiufundi Bw. Ronald Lwakatare kutoka Taasisi ya Mfuko wa Barabara akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Anitha Jonas – MAELEZO)
Na Lorietha Laurence-Maelezo
BODI ya Mfuko wa Barabara nchini(RFB) imefanikiwa kufanya maboresha ya barabara kwa kiwango cha lami katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Serikali ya awamu ya nne wa Mhe. Jakaya Kikwete.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Jana Bw. Joseph Haule amesema kuwa matengenezo hayo yamefanikisha ujenzi wa barabara kuu zinazounganisha mikoa mbalimbali nchini kukamilika kwa asilimia 89 huku zile za Wilaya na Miji kwa asilimia 57.
“ kazi kubwa ya Mfuko huu ni kukusanya mapato kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo tozo za barabarani na ushuru wa mafuta na baadaye kuzigawa kupitia taasisi zinazohusika na ujenzi wa barabara ikiwemo TANROADS, Wizara ya Ujenzi na Ofisi ya Waziri Mkuu “ alisema Bw. Haule.
Aidha aliongeza kuwa Mfuko huo umefanikisha ujenzi wa daraja la Mabatini jijini Mwanza ,daraja la Mwanhunzi na daraja la Mbutu linalounganisha Igunga na Shinyanga pamoja na ununuzi wa vivuko kikiwemo kile cha Mv Malagarasi.
Mbali na hayo Bw.Haule aliongeza kuwa Bodi hiyo inaendelea kuhakikisha barabara zinatunzwa kwa kudhibiti magari ya mizigo yanayozidisha uzito unaochangia uharibifu wa barabara kwa kuanzisha mfumo wa kisasa wa kamera utakaokuwa unaratibiwa na mfuko huo.
Mfuko huo umefanikiwa kuanzisha ujenzi wa barabara kwa kutumia mawe ambao ni wa gharama nafuu na wa kudumu kwa muda mrefu,hata hivyo miradi hiyo imeanza kutekeleza katika mikoa ya Kigoma na Mwanza.
Kutokana na mtandao wa barabara kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara imesaidia kuongeza ubora wa barabara na kupanua wigo wa biashara kati ya Tanzania na nchi za jirani ikiwemo Zambia,Malawi,Burundi,Rwanda na Uganda.
Mbali na mafanikio hayo Mfuko huounakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa bajeti kutokana na fedha zinazopatikana kutokukidhi mahitaji.
No comments:
Post a Comment