Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Neema
Rusibamayila toka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii akizungumza na waandishi wa
habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho
ya wiki ya unyonyeshaji inayotarajiwa kuanza Agosti Mosi hadi Saba ambapo
kitaifa itafanyika mkoani Dodoma. (Picha na Eliphace Marwa-Maelezo)
Na Eliphace Marwa – Maelezo.
KATIKA kuzingatia na kuboresha afya ya mtoto, Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii imeendelea kuwahimiza wanawake kuzingatia utunzaji
na ustawishaji wa watoto kwa kuwapa haki ya kunyonya maziwa ya mama.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya
katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga
Dkt. Neema Rusibamayila amesema wakati Tanzania inategemea kuungana na mataifa
mengine duniani ni vema jamii ikatambua
umuhimu wa lishe kwa mtoto.
“Jamii inapaswa kutambua umuhimu wa unyonyeshaji
maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto na
kuendelea kunyonyeshwa mpaka umri wa miaka miwili au zaidi” alisema Dkt. Neema.
Kwa upande
wa mtoto, Dkt.
Neema alisema maziwa hayo yana faida nyingi ikiwemo kumpatia virutubisho vyote
anavyohitaji kwa uwiano sahihi kwa afya na ustawi kwani viini vya kingamwili
vinavyofanya kazi kama chanjo dhidi ya maradhi humeng’enywa na kufyonzwa
kirahisi zaidi mwilini tofauti na vyakula vingine.
Aidha aliongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu
yataenda sanjari na kilele cha maadhimisho
ya miaka 25 ya Azimio la Innocenti la mwaka 1990ambalo linasisitiza
umuhimu wa kulinda, kuendeleza na kusaidia unyonyeshaji na ulishaji bora wa
watoto.
Mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo yanayotarajiwa
kuanza Agosti Mosi na kufikia kilele chake Agosti 7 mkoani Dodoma katika
viwanja vya Nanenane ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi yakiwa
na kauli mbiu “Unyonyeshaji na kazi,
hakikisha inawezekana” yenye lengo la kuwasaidia wanawake wote wenye ajira
rasmi na zile zisizo rasmi waweze kutunza watoto wao ipasavyo pasipo kuathiri
ajira zao zinazowapatia kipato.
No comments:
Post a Comment