Mkurugenzi wa TanTrade Bi. Jacqueline Maleko
Na Lorietha Laurence, Salma Ngwilizi- Maelezo
RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonyesho ya kimataifa ya sabasaba utakaofanyika Julai 3, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa TanTrade Bi. Jacqueline Maleko ameeleza kuwa maonyesho hayo yameshaanza tangu Juni 28, mwaka huu, ambapo kuna fursa mbalimbali kwa watanzania kujitokeza na kujifunza mambo ya ujasiriamali kutoka kwa wataalam na wafanyabiashara wa nje.
Aliongeza kuwa maonyesho hayo yameshirikisha takribani kampuni 170 kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Japan, India,Italia na Korea ambao wanatoa mafunzo mbalimbali ya namna ya kutumia teknolojia katika kujiletea maendeleo hususani katika sekta ya biashara.
“Naomba wananchi wajitokeze kwa wengi kuhudhuria maonyesho haya isiwe tu kwa kununua bidhaa bali pia kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara wengine ili kuongeza ufanisi katika biashara zao” alisema Bi Maleko.
Aidha alibainisha kuwa Julai 2, mwaka huu kutakuwa na kongamano la kibiashara litakalowapa fursa wafanyabishara wakubwa kwa wadogo kukutana na wamiliki wa kampuni, wazalishaji,wataalam na wafanyabiashara wakubwa kujadili masuala mbalimbali ya biashara.
Vilevile aliongeza kuwa kutakuwa na punguzo la bei ya kiingilio kwa wanafunzi ambapo wataingia kwa shiriki elfu moja ili nao waweze kujifunza mambo mbalimbali katika maonyesho hayo.
Pia kwa upande wa ulinzi Bi. Maleko aliwakikishia wananchi kuwa ulinzi umeimarishwa kwa kuwepo kwa vifaa muhimu vya ukaguzi wakati wa kuingia pamoja na kamera zinazoonyesha yale yote yanayoendele kwenye viwanja hivyo vya sabasaba.
Maonyesho haya ya Kimataifa ni ya 39 tangu yaanzishwe hapa nchini na yamekuwa yakitoa fursa mbalimbali kwa wafanyabiashara wa ndani na nje kuweza kunadi na kuuza bidhaa zao kwa watanzania na wageni.

No comments:
Post a Comment