TANGAZO


Friday, July 31, 2015

NEC yataka amani na utulivu kuzingatiwa

*Yatangaza ratiba ya uchukuaji fomu za kugombea 
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva

Na Magreth Kinabo
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka  viongozi mbalimbali   wa vyama vya siasa watakwenda kuchukua fomu  pamoja na wafuasi  wao kuzingatia suala la amani na utulivu.

Aidha Tume hiyo imewataka viongozi hao kuwa waangalifu na matamshi ambayo yanaweza  kuhatarisha amani na utulivu.

Kauli hiyo, imetolewa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, wakati akizungumza na waandishi habari katika ukumbi wa mikutano wa tume hiyo kuhusu mchakato wa uchukuaji  fomu za wagombea wa kiti cha urais utakaoanza Agosti Mosi mwaka huu. 

Alisema  kila mwananchi anayohaki na uhuru wa kushiriki shughuli za utawala wa nchi ikiwa ni pamoja haki ya kuchagua na kuchaguliwa au kuanzisha na kujiunga na vyama vya siasa kama ilivyo katika Ibara za 20 na 21 za Katiba ya mwaka 1977.

 Jaji Lubuva aliongeza kwamba shughuli hizo kwa mujibu wa Katiba zimewekewa mipaka chini ya Ibara ya 30 ya Katiba. Kwamba, haki  ya kushiriki isifanywe kwa namna  ya kuingilia kati au kukatizwa  kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma. 
 
Alisema shughuli zinazoanza kesho na siku zinazofuata za kuchukua fomu vyama vyote ni lazima zifuate na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Sheria.
  
 Hivyo lengo ni kuhakikisha kuwa mchakato wote tangu mwanzo wa kuchukua fomu na kuzirudisha na baadaye yatakayofuata hadi mwisho wa kampeni na kupiga kura unafanyika kwa amani na utulivu nchi nzima.

“Viongozi mbalimbali wanaokuja kuchukua fomu  kutoka tume , waje kwa amani na waondoke kwa amani pamoja na wafuasi wao.

“Shamrashamra zitakazoambatana nao zisiwe chanzo   cha vurugu au kusababisha adha kwa wananchi wengine. Uchaguzi si ugomvi kati ya wagombea au wafuasi wao. Vinginevyo sheria itachukua mkondo wake,” alisema  Jaji Lubuva.

Aidha, tume hiyo imewakuambusha wagombea hao na vyama vyama vyao kuzingatia maadili ya uchaguzi yaliyotiwa saini Julai 27, mwaka huu.

 Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar esSalaam Kamishna Suleiman Kova alisema jeshi hilo liko katika mkakati wa  hali ya juu ya kuhakikisha uchaguzi ufanyika kwa amani na usalama, hivyo halivumilia vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani, hatua kali za kisheria zitaweza kuchukuliwa.

 Kamanda Kova aliongeza kwamba shughuli za kijamii zitaendelea kama kawaida wakati wa uchukuaji fomu.

 Alisema wagombea hao pamoja na wafuasi wao watatakiwa kutumia barabara ya Oboma hadi klabu Jimy Cana jijini Dar es Saam ambapo watawaacha  washabiki wao  baada ya kuchukua fomu watawapitia  ili kuweza kupunguza msongamano.

Jaji Lubuva aliongeza kuwa  kesho wagombea wa kiti cha urais kutoka  vyama vitatu watafika NEC kuchukua fomu, ambao ni  UPDP saa 3:00 asubuhi, TLP saa 6:00 mchana na DP saa 8:00 mchana.

Alivitaja vyama vitakavyofuata kuwa ni  Agosti 4, mwaka huu na  Agosti 5, mwaka huu  kuwa ni  ADC  saa 3:00 asubuhi na TADEA saa 4:00 asubuhi.

Akizungumzia kuhusu ratiba ya uchukuaji fomu, kwa wagombea wa kiti cha urais, ubunge na udiwani, Mkuu wa Idara ya Uendeshaji kutoka NEC  Clothilde Komba  alisema inaanza Agosti Mosi, mwaka huu na kumalizika Agosti 21,mwaka huu saa 10:00 jioni.

No comments:

Post a Comment