MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (pichani), ameahidi kusomesha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu 12, ikiwa ni kuwalipia ada za shule.
Hayo aliyabainisha Dar es Salaam jana wakati Kampuni ya Simu za mkononi Zantel ikikabidhi kisima cha maji safi katika kituo cha kulea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu cha Watoto Wetu Tanzania kilichopo Mbezi Suka jijini Dar es Salaam.
Watoto hao 12, ambapo 8 kati yao wana elimu ngazi ya sekondari huku 3 wakitakiwa kwenda chuo kikuu na 1 kuahidiwa endapo atafaulu kidato cha nne sanjari na kuongea na mifuko ya hifadhi za jamii kuona jinsi gani wanaweza kusaidia kundi hilo katika huduma za afya.
Makonda alisema familia ni chanzo cha kuongeza idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu kutokana na ugumu wa maisha, kuoana katika umri mdogo na uelewa mdogo wa maana ya familia.
"Familia ni chanzo kizuri cha kuongeza au kupunguza idadi ya watoto wa mitaani, familia nyingi hazina uvumilinu ndani ya ndoa zao...msijitazame kama yatima kwasababu hamtaweza kuwa na maendeleo mazuri,"alisema Makonda.
Kwaupande wake Mkurugenzi mtendaji Kampuni ya Zantel, Pratap Ghose alisema kampuni hiyo imekuwa ikionesha jitihada za kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwenye jamii inayoizunguka.
"Kampuni yetu inalenga kugusa maisha ya wananchi wanaotuzunguka, na ndio maana tumeamua kutoa msaada wa kisima ili kiweze kukisaidia kiyuo hiki kumaliza moja ya matatizo yaliyokuwa yanawakabili kwa muda mrefu,"alisema Ghose.
Mkuu wa kituo cha Watoto Wetu Tanzania, Evance Tegete alisema awali kituo kilikuwa kinategemea maji kutoka Dawasco ambayo upatikanaji wake ulikuwa si wa uhakika, hivyo wanaishukuru kampuni hiyo kwa kuwachimbia kisima hicho.
Kituo cha Watoto Wetu tanzania kilianzishwa mwaka 2001,ambapo hadi sasa kina watoto 70, kuanzia umri wa miaka 5 hadi 25 kutoka mikoa mbalimbali kikiwa na lengo la kuhakikisha watoto wasio na wazazi au walezi wanapata matunzo na elimu bora. ((Imeandaliwa na Dotto Mwaibale)
No comments:
Post a Comment