Kambi hasimu nchini Ugiriki zinatarajiwa kufanya mikutano mikubwa ya hadhara mjini Athens kabla ya kura ya Maamuzi hapo Jumapili, kuamua masharti ya kupokea mkopo kutoka kwa wakopeshaji wa kimataifa.
Waziri Mkuu Alexis Tsipras anatarajiwa kuongoza mkutano wa mrengo wa 'La' ambao unapinga masharti ya kupewa ufadhili.
Viongozi wa Muungano wa Ulaya wameonya kura ya 'La' huenda ikapelekea Ugiriki kuondoka katika kanda inayotumia sarafu ya Euro.
Ugiriki imeshindwa kuafikiana na wakopeshaji wake kwa miezi kadhaa na ililazimika kuitisha kura ya maamuzi wiki jana. Kila upande umekua mbioni kupata eneo la mkutano wake mjini Athens.
Mikutano yote itafanyika kati kati mwa Athens kila upande ukijaribu kuwashawishi wafuasi wake kuhusu kura hii ya maamuzi.
Kumekuwa na maandamano kadhaa katika siku za karibuni baadhi yakikumbwa na vurugu kati ya waandamanaji na polisi.
Wakati huo huo mahakama ya juu Ugiriki inatarajiwa kuamua ikiwa ni halali kura hiyo kufanyika siku ya Jumapili.

No comments:
Post a Comment