TANGAZO


Tuesday, July 21, 2015

Mbunge wa Kahama James Lembeli aondoka CCM na kujiunga rasmi na Chadema


Aliyekuwa Mbunge wa Kahama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), James David Lembeli (kushoto) akiingia ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl Ubungo Dar es Salaam leo asubuhi akiwa ameongozana na mtoto wake, Wizilya Lembeli wakati akienda kutangaza kuondoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kahama mkoani Shinyanga, James David Lembeli, akizungumza na waandishi wa habari Hoteli ya Blue Pearl Ubungo Dar es Salaam leo asubuhi wakati akitangaza kuondoka katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Pamoja na kutangaza nia ya kugombea ubunge kupitia chama hicho. Lembeli akizungumza na wanahabari.Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.Wanahabari wakimsikiliza Lembeli. Suleiman Msuya
Na Mwandishi Wetu

ALIYEKUWA Mbunge wa Kahama James Lembeli, amehamia rasmi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Tukio hilo la kuhama lilifanyika jijini Dar es Salaam leo asubuhi katika Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza ambapo aliambatana na mwanae ambaye alijitambulisha kwa jina Wizilya James.



Akizungumzia uamuzi wake huo Lembeli alisema amekuwa ndani ya CCM kwa miaka yake yote lakini kutokana na vitendo vinavyofanyika ndani ya chama hicho ameaona akae pembeni.



Lembeli alisema, ndani ya CCM ili ufanikiwe kupita michakato yote sahihi ni lazima utoe rushwa au kuiba kura jambo ambalo yeye analipiga vita hivyo kutofautiana na viongozi wa chama ngazi ya Wilaya.



"Ndani ya CCM rushwa imekuwa ibada inasumu kali kuliko ukimwi hivyo nimeshindwa kuvumilia naona Chadema wana viashiria vinavyofanana na mimi ngoja tukafanye kazi," alisema Lembeli.



Alisema katika harakati za kupata wagombea katika jimbo la Kahama kila mwaka ni lazima rushwa itumike lakini chama kimekuwa kimya na kuwabeba wale watoa rushwa.



Mbunge huyo alisema ushahidi wa watu kutoa rushwa hasa katika kipindi hiki umeonekana lakini wahusika wameendelea na hatua zingine bila kukemewa.



"Mimi mwaka 2010 nilikuwa nimekatwa lakini huruma ya Rais Jakaya Kikwete nilirejeshwa sasa nimeona hakuna sababu ya kuendelea kulazimisha kama viongozi hawakutaki," alisema.



Alisema iwapo angechukua fomu CCM mkakati ambao ulikuwepo ni kumkata kwa kile ambacho wanaamini kuwa amekuwa akisimamia misimamo ambayo ina madhara kwa Serikali.



Lembele alisema kutokana na dhana hiyo ni vema aende katika chama ambacho kinaonekana kuwa wabunge wake wanauchungu na nchi yao na sio kubebana kusiko na sababu.



"Kufanya kosa sio kosa lakini kurudia kosa ni kosa kubwa sana hivyo siwezi kurudia kosa la 2010 hivyo huku Chadema ndiko sahihi," alisema.



Alisema ukiona mwenzako ananyolewa ni vema kujiandaa kwa kutia maji nywele jambo ambalo ameliona na ameamua kufanya hivyo.



"Siwezi kutoa rushwa kwa sababu sijafunzwa hivyo na hata wananchi wa Kahama wanajua kuwa mimi sio mtoa rushwa hivyo ukiwa hutoi rushwa CCM ni ngumu kukubalika jambo ambalo linafanya kuwa rushwa iwe mbaya kuliko ukimwi," aliongezea.



Akizungumzia kugombea ubunge kupitia Chadema, alisema atafanya hivyo kwani ukweli ni kuwa anakubalika kwa wananchi wote kutokana na misingi yake ya utumishi.



Alisema mpaka anafanya uamuzi huo ameshafanya utafiti ambapo anaamini kuwa atashinda tena kwa kishindo kwani wananchi wa jimbo hilo wanamkubali.



Lembeli alisema kimsingi jimbo la Kahama wapinzani wapo tangu yeye akiwa Mbunge, hivyo anaamini kuwa iwapo atafanikiwa kushinda hatapata wakati mgumu kufanya kazi.



"CCM imefanya mambo mengi ambayo kimsingi hayana afya ndani ya chama ukiwa wa kwanza kwa kura ndani ya CCM unakuwa wa mwisho hali ambayo inakatisha tamaa na hilo lilitokea 2010 na Chadema wakapata ushindi," alisema



Pia alisema amepokea simu na meseji nyingi ambazo kutoka kwa wananchi zinamtaka agombee kupitia chama Chadema hivyo pamoja na ukweli kuwa ni uamuzi mgumu ila hawezi kula matapishi.



Alisema ilimchukua masaa 10 kumuelezea mama yake juu ya uamuzi huo lakini baadae alielewa hivyo kwa sasa ana baraka zote za mama na familia kwa ujumla.



Kuhusu uhusiano na 4U Movement
Akizungumzia kuhusu uamuzi huo kuhusishwa na kundi la 4u Movement, alisema kimsingi kundi hilo analiona kupitia mitandoa ya kijamii ila hana uhusiano nalo na hahitaji kuwa katika hao.



Lembeli alisema wananchi wa Kahama ni watu makini wanajua nini cha kufanya hivyo uamuzi ambao watafanya utakuwa ni kwa uelewa wao na sio kwa msukumo wa kundi hilo linalotajwa kuwa ni wafuasi wa Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa.



Kuhusu Katiba iliyopendekezwa Lembeli alisema yeye ni muumini wa Serikali tatu na alionesha hilo katika vikoa vyote vya bunge lile ambapo alikuwa katika kamati namba moja.



Alisema kutokana na ukweli huo ni dhahiri kuwa ameenda chama ambacho wanafanana kifra kwani bila Serikali tatu hatma ya Tanzania itakuwa mashakani.



"Kwa hili siwezi kubadilika mimi msimamo wangu hadi leo ni Serikali tatu ambapo pia ni msimamo wa Chadema hivyo wengi ndio walishinda lakini mimi sio mmojawapo," alisema.



Aidha Lembeli alitumia muda huo kufafanua ni kwanini alitoa hoja ya kutaka Lowassa na wengine ambao wamekutana na majanga ndani ya bunge wasafishwe ambapo alisema haki haikutendeka kusafisha watu baadhi na wengine kuachwa.



Lembeli alisema katika taarifa ya Operasheni Tokomeza haikusema mawaziri fulani wanamakosa ila iliweka bayana kuwa kulinga na nafasi zao wanapaswa kuwajibika kisiasa.



Alisema mfumo wa kusafisha watu fulani na wengine kuwaacha sio mzuri kwani hauendani na misingi ya haki za binadamu ni ubaguzi.



Kwa upande wa mtoto wake wa pili Wizilya James Lembeli alisema wanamuunga mkono baba yao kwa uamuzi huo na kuwa wako nyuma yake.



Alisema uamuzi ambao amechukua baba yake ni mgumu hasa ukilinganisha na kipindi husika lakini hakuwa na njia nyingine kwani ni mtu wa siasa.



Akizungumzia ujio huo Ofisa Habari wa Chadema ambaye ndiye alimpokea Lembeli alisema kimsingi mwanachama huyo mpya alikiwa ni mpinzani kiroho hivyo hawana shaka naye.



Makene alisema wanaamini kuwa wamepata mtu ambaye anapenda mabadiliko kwani alionekana ndani ya bunge na nje kwa kusimamia rasilimali za nchi bila uoga.



Alisema Chadema itaendelea kupokea wanachama wapya kutoa CCM na vyama vingine hadi Julai 25 kwani lengo lao ni kuhakikisha kuwa nchi inafikia kwenye mabadiliko chanya.



Lembeli amekuwa Mbunge wa jimbo la Kahama, tangu mwaka 2005 hadi 2015 ambapo awali alikuwa  mwandishi na mtumishi katika shirika la Hifashi ya Taifa (Tanapa).(Imeandaliwa na Dotto Mwaibale)

No comments:

Post a Comment