MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imewataka wananchi wenye malalamiko kuhusu vitendo vya rushwa mahakamani kutoa ushirikiano ili kuweza kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.
Hayo yalisemwa katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini Dar es salaam na Afisa Habari Mary Gwera wa Mahakama hiyo kufuatia gazeti moja la hapa nchini la Julai 21 mwaka huu kupitia makala yenye kichwa cha habari “Mtandao wa rushwa Mahakamani huu hapa” .
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, baada ya kufanya uchunguzi juu ya kesi zilizoandikwa katika makala hiyo Mahakama haikuweza kupata maelezo sahihi kuhusu kesi mbalimbali za watu wenye malalamiko hayo ambao ni Muhidini Nguluma ,Kuruthum Majjid, Abadallah Majata, Halima Abdan, Claudiana Mbazigwa Mpondela na Laizer Kaanan.
“Ili kuondoa kero zilizobainishwa katika gazeti la Mwananchi , mahakama inatoa rai kwa gazeti la Mwananchi au mtu yoyote mwenye taarifa sahihi kuipatia ushirikiano ili kupata namba za simu za kesi zilizolalamikiwa na mahakama zilikofunguliwa,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha mahakama hiyo imeomba wale wote waliotajwa katika makala hiyo wafike Makao Makuu ya Mahakama, Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Namba 11409 Kivukoni Front waonane na Mkurugenzi Msaidizi wa Malalamiko katika Idara ya Ukaguzi wa Huduma za Mahakama na Maadili ili watatuliwe kero zao.
Mahakama hiyo inasisitiza kwamba imeweka namba za simu 0752–500 400. mitandao ya kijamii, WhatsApp, na barua pepe info@judiciary. go.tz) ili wananchi na wadau mbalimbali waweze kutoa malalamiko yao, maoni na mapendekezo.
No comments:
Post a Comment