TANGAZO


Tuesday, July 21, 2015

Kongamano la kuhamasisha ushiriki wa Diaspora katika kukuza biashara ndogo na za kati kufanyika nchini

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Diaspora kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bi. Rosemary Jairo akiongea na waandishi wa Habari kuhusu Maandalizi ya Kongamano la Diaspora (Tanzania and SMEs Partnership Conference 2015) litakalofanyika kuanzia tarehe 13-15 Agosti 2015 Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (Maelezo), Leo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waandishi wa Habari wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Idara ya Diaspora kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bi. Rosemary Jairo.  (Picha zote na Hassan Silayo-Maelezo)

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji cha Kimataifa (International Trade Centre UN-Agency) inafanya Maandalizi ya Kongamano la Diaspora (Tanzania Diaspora & SMEs Partnership Conference 2015). 
Kongamano husika litafanyika hapa Dar es Salaam, kuanzia tarehe 13 hadi 15 Agosti 2015 katika Hoteli ya Serena. Kongamano hilo litakuwa la pili kufanyika hapa nchini na litahusisha Diaspora na Wadau wa hapa Tanzania.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ofisi ya Rais na Utawala Bora – Zanzibar na Ofisi ya Waziri Mkuu ndio Wadau Wakuu katika Maandalizi ya Kongamano hili.
Kongamano la mwaka huu lina Kauli Mbiu, ‘Creating Linkages between Diaspora and Local SMEs in Tanzania’ na Dhumuni lake ni kuhamasisha Ushiriki wa Diaspora katika kukuza Biashara Ndogo na za Kati hapa nchini. Kongamano la mwaka huu pia litahusisha Mikoa ya Tanzania ambapo Mikoa itapata fursa ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo Mikoani.

Kongamano hilo linatarajiwa kufunguliwa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufungwa na Mhe. Dr. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Aidha, katika kuhitimisha kilele cha Kongamano hilo, Diaspora wanatarajiwa kufanya ziara Zanzibar tarehe 15 Agosti 2015, ikiwa ni sehemu ya mwaliko maalum kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Pamoja na Shughuli za Ufunguzi na Kilele, Matukio muhimu yatakuwa ni Maonesho ya Kibiashara, Majadiliano ya Mada kuhusu Ushirikishwaji wa Diaspora kwa Maendeleo ya Nchi hususan SMEs, uwekezaji Mikoani n.k.
Kongamano hilo litahudhuriwa na Watanzania Wanaoishi Ughaibuni (Diaspora) na wale waliorejea hapa nchini na Wadau wa Maendeleo kutoka hapa nchini.

Wizara ya Mambo ya Nje inawakaribisha kushiriki nasi katika Kongamano hilo. Tafadhali tembeleeni tovuti ya (www.tzdiaspora.com) kupata taarifa muhimu hususan kuhusu Ada za Ushiriki, fursa za Kufadhili na namna ya kujisajili.

Imetolewa na: Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam
21 Julai

No comments:

Post a Comment