Diwani wa Wadi ya Upenja Bibi Asha Abdulla akimshukuru na Kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif hayupo pichani kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kutekeleza ilani ya CCM katika kipindi cha uongozi wake wa miaka 10 ndani ya Jimbo hilo.
Sheha wa Shehia ya
Kilombero Bwana Muhammad aki[pokea msaada wa Tangi kutoka kwa Mbunge wa Jimbo
la Kitope Balozi Seif kwa ajili ya kuhifadhia maji safi ytakayotumiwa na
wananchi wa Kijiji cha Kilomberi Wilaya ya Kaskazini “B”. (Picha zote na Hassan Issa
–OPMR – ZNZ)
Na Othman
Khamis Ame
Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
3/7/2015.
Mbunge wa
Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi amewanasihi wananchi wa jimbo hilo kuelewa
kwamba jukumu na wajibu wa kulinda miradi yao ya Maendeleo waliyoianzisha wao
wenyewe na ile iliyopata msukumo wa Serikali Kuu kwa kushirikiana na washirika
wa maendeleo limo ndani ya mikono yao.
Amesema wapo
watu katika baadhi ya maeneo hapa nchini huamua kuiharibu miundombinu kwa
utashi wao ambayo imeanzishwa kwa ajili
ya kuwahudumia Wananchi walio wengi bila
ya kufikiria usumbufu utakaowapata wana Jamii hao hapo baadaye.
Balozi Seif
Ali Iddi alisema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi Mipira kumi ya kusambazia
maji safi na salama pamoja na Tangi la Kuhifadhia maji kwa ajili ya Wananchi wa
Kijiji cha Kilombero hapo katika Tawi la Chama cha Mapinduzi Kilombero Wilaya
ya Kaskazini “B”.
Mipira
pamoja na Tangi hilo vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi Milioni Tatu
ni utekelezaji wa ahadi aliyowapa Wananchi wa Kilombero wakati alipokuwa
akizindua Mradi wa Maji safi na salama wa Kijiji hicho katika wiki za hivi
karibuni.
Balozi Seif
aliwaeleza Wanachama hao wa CCM pamoja na Wananchi wa Kilombero kwamba huduma
za maji safi na salama zinazoendelea kuimarishwa na Serikali Kuu kwa kushirikiana
na washirika wa Maendeleo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010
inayokaribia kumaliza muda wake mwaka huu wa 2015.
“Maji ni
uhai na maisha ya kila siku yanayomstahikia kupata kila kiumbe wakiongozwa na
Mwanaadamu na ndio maana yakatiliwa mkazo ndani ya Ilani ya CCM “. Alifafanua
Balozi Seif.
Mbunge huyo
wa Jimbo la Kitope aliwahimiza na kuwakumbusha Wananchi hao wajitokeze kwa
wingi kupiga kura wakati utakapowadia kwa kuwachagua Viongozi wote
watakaosimamishwa na Chama cha Mapinduzi ambao ndio wenye uwezo kamili wa kulinda
amani na utulivu wa Taifa.
Balozi Seif
alitahadharisha kwamba wakati wa kuwachagua Viongozi vibaka, matapeli na
wababaishaji kwa hivi sasa umepitwa na wakati kutokana na mfumo na mbadiliko ya
Dunia uliopo hivi sasa.
Mapema Diwani
wa Wadi ya Upenja Bibi Asha Abdulla alisema Wananchi wa Kijiji cha Kilombero
wamemuhakikishia Balozi Seif kumuunga mkono kwenye harakati zake za kuendelea
kuwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Kitope wakati utakapowadia.
Diwani Asha
alisema Balozi Seif akiwa Mbunge wa Jimbo la Kitope kwa takriban miaka kumi
sasa tokea mwaka 2005 amefanya mengi ya Maendeleo ndani ya uongozi wake katika
kuwahudumia wananchi wa Jimbo hilo.




No comments:
Post a Comment