TANGAZO


Tuesday, June 2, 2015

Rais Dk. Shein ziarani Ujerumani

Rais wa zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Ramadhan Othman, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameondoka nchini leo kwenda nchini Ujerumani kwa ziara ya kikazi ya siku nane.

Akiwa nchini humo siku ya Alhamisi ijayo, Dk. Shein atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Muziki yanayofanyika katika mji wa Wurzburg pamoja na kuhudhuria utoaji wa zawadi kwa mwaka 2015.

Zanzibar inashiriki katika Maonesho hayo yanayofanyika kila mwaka ambayo yanajumuisha wanamuziki na wasanii mashuhuri kutoka nchi za kiafrika pamoja na nchi za mabara mengine ulimwenguni.

Siku inayofuata Dk. Shein atakutana na kufanya mazungumzo na Mstahiki Meya wa Wurzburg na baadae atatembelea Taasisi ya Utibabu ya mji huo(Medical Mission Institute).

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ataendelea na ziara yake nchini humo ambapo siku ya Jumapili tarehe 07 Juni, 2015 atakwenda katika mji wa Frankfurt ambako jioni atakutana na watanzania wanaoishi nchini Ujerumani.

Siku inayofuata atakwenda katika mji wa Postdam ambako atatembelea skuli ya msingi ya Bruno-H-Burgel ambayo ina ushirikiano na skuli ya Mwanakwerekwe Unguja. Siku hiyo hiyo jioni atakutana na mabalozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walioko nchini Ujerumani.

Tarehe 09 Juni, 2015 Dk. Shein atakutana na wanachama wa Chama cha Wafanyabiashara wa Ujerumani ambako atatoa hotuba rasmi.

Katika ziara hiyo Dk. Shein amefuatana na mke wake Mama Mwanamwema Shein, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk, Waziri wa Kilimo na Maliasili Dk. Sira Ubwa Mamboya, Naibu waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dk. Mahadhi Juma Maalim na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.

Wengine ni Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa na Katibu Mkuu wizara ya Biashara,Viwanda na Masoko Julian Banzi Raphael.

Dk Shein wake anarajiwa kurejea nchin tarehe 10 Juni, 2015.

Katika uwanja wa ndege wa Zanzibar Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliagwa na viongozi mbalimbali wa serikali wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.
  

No comments:

Post a Comment